Kuoga mara mbili kwa siku na kupunguza pombe kumenifanya nimekuwa afadhali - Brian Chira

Hata hivyo, Chira alisema kwamba yeye kubadilika haina maana kwamba atanyong’onyea pindi watu watakapomchokoza na kuingia kwenye anga zake.

Muhtasari

• Alisema kwamba ujio wake katika Sanaa ya burudani utakuwa mkubwa na si tu kwenye TikTok bali anatarajia kuzindua podkasti yake kwenye YouTube pia.

•Lakini pia alisema katika ujio wake, hatoweza kuifanya shoo yake pasi na kubugia japo moja chupa ya kumpunguzia mawazo na kumpa mihemko ya kuhimili mashabiki wake.

Brian Chira
Brian Chira
Image: Screengrab

TikToker Brian Chira ameibuka baada ya kimya kirefu katika mitandao ya kijamii na kukiri kwamba hajakuwa sawa kiakili katika kipindi cha siku kadhaa.

Chira ambaye mwaka jana alikuwa anagonga vichwa vya habari kutokana na vituko vyake kwenye mtandao wa TikTok alichimba mitini asiweze kusikika tena kwa kipindi cha siku kadhaa, baadhi wakisema kwamba huenda alikuwa anasumbuliwa na unyungovu.

Akizungumza na YouTuber Nicholas Kioko, Chira alikiri kwamba ni kweli hajakuwa sawa kiakili lakini akasema kwamba katika kipindi ambacho ametoweka mitandaoni, amekuwa akihudhuria vipindi vya kurekebika kitabia na mtaalamu wa masuala ya akili.

“Sikuwa vizuri kiakili, huo nao sio uongo na nimekuwa nikionana na mtaalamu wangu, shukrani sana kwake,” Chira alisema.

Kijana huyo ambaye aliwahi kukiri wazi kuwa mwathirika wa virusi vya HIV alifichua baadhi ya vitu ambavyo amelazimika kuvibadilisha katika mzunguko wake wa maisha ya kila siku ambavyo kwa namna moja au nyingine vimemboresha.

“Nimekuwa nikijaribu kujiboresha, kujipenda kwanza, kupunguza chupa [mvinyo], kujilinda mwenyewe kama vile kuoga mara mbili kwa siku, unajua vitu kama hivyo vimekuwa vikinifanya nikuwe afadhali,” alisema.

Hata hivyo, Chira alisema kwamba yeye kubadilika haina maana kwamba atanyong’onyea pindi watu watakapomchokoza na kuingia kwenye anga zake.

“Huyu Chira bado ana vituko vyake, mimi ukinijia hata kama wewe ni mkubwa aje kwenye Sanaa ya showbiz, aai mimi nitakukujia pia. Si eti nitanyamaza eti kisa ninajijenga upya, nikisikia mtu ananiongelea vibaya name nitamwendea vivyo hivyo,” Chira alikula yamini.

Alisema kwamba ujio wake katika Sanaa ya burudani utakuwa mkubwa na si tu kwenye TikTok bali anatarajia kuzindua podkasti yake kwenye YouTube pia.

Lakini pia alisema katika ujio wake, hatoweza kuifanya shoo yake pasi na kubugia japo moja chupa ya kumpunguzia mawazo na kumpa mihemko ya kuhimili mashabiki wake.

“Nitakuja na maudhui yangu kwenye YouTube yatakuwa kama Podkasti, yangu haitakuwa imetulia vile, lazima nipige shots [pombe] kidogo halafu tuingie tupige shoo. Unafikiri kuzungumza kwa dakika 40 ni mchezo, lazima upige kidogo,” Chira alisema.