Muigizaji mkongwe wa Bongo Irene Uwoya aanzisha kanisa lake,"Baba nimeitikia wito"

Wasanii wengine ambao waliasi mitindo ya kidunia na kwa sasa ni wahudumu wakubwa wa injili ni pamoja na Lovy Longomba kutoka kundi la Longombas nyakati hizo, Size 8 miongoni mwa wengine.

Muhtasari

• Mwaka mmoja uliopita, Uwoya alionesha dalili za kujiweka karibu kabisa na kanisa baada ya kupata mwaliko rasmi kuhudhuri kikao cha kina mama katika kanisa moja.

Irene Uwoya
Irene Uwoya
Image: Instagram

Muigizaji mkongwe wa filamu za Kiswahili kutoka Tanzania, Irene Uwoya amekiri kuitikia wito wa Mungu kuokoka na kuwa mchungaji kulinadi neno.

Muigizaji huyo ambaye katika kipindi cha miaka miwili iliyopita amekuwa akionesha dalili za kuokoka na kujitenga na maisha ya kidunia hatimaye ameweka wazi kwamba ameukubali wito.

Uwoya kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha picha yenye nembo ya jina linalokisiwa kuwa ni la kanisa lake jipya ambalo anawazia kulizindua hivi karibuni.

Uwoya alikwenda mbali Zaidi na kuitumia nembo hiyo kwenye picha yake ya utambulisho katika ukurasa huo, ishara kwamba ameshaamua kabisa ni kuhudumia kanisa na si vinginevyo.

“Baba nimeitika…” Uwoya aliandika kwenye picha hiyo.

Mashabiki wake wengi walisimama naye katika hilo wakimwambia kwamba ndio uamzui sahihi wa kuuchukua.

Wengi katika upande wa kutoa maoni walimtaja kama ‘Mama Mchungaji’ na kumtaka asiaibike kuifuata ndoto yake mpya.

Mwaka mmoja uliopita, Uwoya alionesha dalili za kujiweka karibu kabisa na kanisa baada ya kupata mwaliko rasmi kuhudhuri kikao cha kina mama katika kanisa moja.

Mchungaji wa kanisa hilo kwa jina Bishop Geography Bendera kwenye ukurasa wake wa Instagram alitangaza kwamba wanawake ni jeshi kubwa na hivyo jumapili hiyo kanisa lake la ufunuo lililoko jijini Morogoro lilikuwa na ibada maalum kuwasherehekea wanawake na pia kuambatana na sherehe za kuadhimisha miaka 8 tangu aanze kutoa huduma kwa kondoo wa bwana.

“Wamama ni jeshi kubwaaaa, Jumapili hii mama wa Ufunuo Morogoro, wana jambo Lao, wakiwa na mwanamama mchapa kazi,mjasiriamali,super women @ireneuwoya8 kama mgeni rasmi,” aliandika askofu Bendera.

Hata hivyo, Uwoya si msanii wa kwanza kutoka Bongo kudai kwamba anawazia kuwa mchungaji.

Wiki jana tuliripoti kwamba muigizaji Tunda ambaye ni mzazi mwenziwe na Whozu aliwauliza mashabiki wake maoni kuhusu yeye kutaka kuwa mchungaji na kuanzisha kanisa lake.

Tunda alionesha shaka yake kuu kuhusu kutoaminiwa na mashabiki wake na pia kuhusu suala zima la kutoa sadaka kwa uaminifu.

Wasanii wengine ambao waliasi mitindo ya kidunia na kwa sasa ni wahudumu wakubwa wa injili ni pamoja na Lovy Longomba kutoka kundi la Longombas nyakati hizo, Size 8 miongoni mwa wengine.