Usitumie miezi 11 kwenye maombi kuombea mwenzi – Burale ashauri watu wa miaka 40+

“Kumbuka nafasi zako sio nyingi kama ilivyokuwa wakati ukiwa na miaka ishirini…Muda wa kila siku unayoyoma ...." alishauri zaidi.

Muhtasari

• Jambo la kwanza, Burale aliwashauri watu wenye umri wa miaka 40 kwenda mbele kutotumia muda wao mwingi katika vituo vya maombi ya kuombea wapenzi kujileta.

Israel ROBERT BURALE
Israel ROBERT BURALE
Image: Facebook

Mshauri wa maisha na ndoa, Israel Robert Burale ametoa ushauri kuntu kwa wanaume na wanawake ambao wanatafuta wapenzi wa kuoana nao na ambao wana umri wa miaka 40 kwenda mbele.

Burale ambaye pia anajiongeza kama mchungaji alitoa hoja kuu 3 kuhusu ni kwa nini watu wenye umri huo wanapitia wakati mgumu wa kupata wapenzi na kuwapa ushauri wa ni nini cha kufanya ili kurahisisha mchakato mzima wa kupata ndoa.

Jambo la kwanza, Burale aliwashauri watu wenye umri wa miaka 40 kwenda mbele kutotumia muda wao mwingi katika vituo vya maombi ya kuombea wapenzi kujileta.

Badala yake, aliwashauri ni bora watenge muda wao na kujumuika na watu wenye jinsi tofauti na zao katika mitoko na kujivinjari – kwa maana hii, ni haraka na rahisi kupata mpenzi kuliko kushinda katika kituo cha maombi kuombea muujiza wa mpenzi kujitokeza kwako ghafla.

“Kwa Mkristo mwanamume au mwanamke aliye na umri wa zaidi ya miaka 40...na kumtumaini Mungu kwa ndoa.... MAOMBI ni muhimu lakini matendo yanahitajika. Usipitie miezi 11 kwenye kituo cha maombi kumwombea mchumba ...Tenga muda wa kwenda kuchumbiana ...yawaaaaa..” Burale alishauri.

Pili, Burale alisema kwamba nafasi za watu wenye umri huo ni finyu kuliko za watu wenye umri ‘mbichi’ na hivyo kuwataka kukumbatia nafasi ndogo ijayo upande wao bila kuharibu muda Zaidi.

“Kumbuka nafasi zako sio nyingi kama ilivyokuwa wakati ukiwa na miaka ishirini…Muda wa kila siku unayoyoma ....ni kama uko kwenye dakika ya 85 ya mchezo wa dakika 90 ....Bwana tusaidie kuzihesabu siku zetu,” alihitimisha.

Awali, Burale aligusia suala la makanisa mengi kuwapa nafasi nyingi wachekeshaji kutumia muda wa mahubiri kuwachekesha waumini ambao wengi wao hawajaenda makanisani kwa ajili ya vichekesho bali kwa ajili ya kuhubiriwa neno.

Pia alisema kuwa baadhi ya wanamuziki wanaojiita wainjilisti nyimbo zao hazifai hata kidogo kukaribia maeneo ya ibada, jambo ambalo alisema ni wakati sasa nyimbo hizo zikashifiwe hadharani.