Akothee ahadithia kisa cha aibu wakati 'aliiba' sidiria ya mamake kwenda kupigwa picha nayo

“Baada ya kupoteza uzito, ilibidi niweke magazeti ndani ya sidiria ili kuiga umbo la matiti. Kwa bahati mbaya, magazeti yalianguka hadi kiunoni mwangu wakati wa upigaji picha..." Akothe alihadithia.

Muhtasari

• Alhamisi ikiwa ni siku ya TBT ambapo watu wengi kupiga kisengere-nyuma kutathmini maisha yao, Akothee hakuachwa nyuma.

Akothee
Akothee
Image: Facebook

Msanii ambaye ni chapa kubwa Zaidi ya kijasiriamali nchini Esther Akoth Kokeyo, maarufu kama Akothee ameibua kumbukumbu za siku za awali wakati alikuwa hana kitu.

Alhamisi ikiwa ni siku ya TBT ambapo watu wengi kupiga kisengere-nyuma kutathmini maisha yao, Akothee hakuachwa nyuma.

Alipakia picha yake ya zamani na kutoa moja ya simulizi ya kutia huruma jinsi alikuwa mpenzi wa sidiria lakini hakuwa na uwezo wa kumudu kupata angalau moja.

Mama huyo wa watoto watano alifunguka kwamba kwa kuwa na mapenzi makubwa kwa sidiria bila uwezo wa kumudu kupata moja, aliamua kuchukua moja ya mamake kwa ajili ya kupigwa picha baada ya ibada ya sabato.

“Wakati mmoja nilivutiwa sana na sidiria lakini sikuweza kumudu. Kwa hiyo, niliamua kuchukua sidiria ya mama yangu kwa ajili ya siku maalum ya Sabato.”

Akothee alisema kwamba kipindi hicho alikuwa amekata uzani wa mwili wake na hivyo sidiria ya mamake haingemtosha, aliamua kuongeza makaratasi ya magazeti yaliyobondwa ndani yake ili kuleta muonekano wa maziwa, lakini tukio hilo halikwenda sawa kipindi cha kupigwa picha.

“Baada ya kupoteza uzito, ilibidi niweke magazeti ndani ya sidiria ili kuiga umbo la matiti. Kwa bahati mbaya, magazeti yalianguka hadi kiunoni mwangu wakati wa upigaji picha, na sikuweza kurekebisha mbele ya kamera. Pamoja na hayo, nilivumilia na kuendelea na shughuli ya upigaji picha,” Akothee alihadithia.

Licha ya kupitia maisha magumu kipindi hicho, Akothee alijikusanya na kujikung’uta mavumbi ambapo aliipata nyota yake katika muziki na kisha baadae akatimba kwenye ujasiriamali alikoanzisha kampuni ya kitalii, Akothee Safaris.