Nyakati tofauti DJ Joe Mfalme alijipata kwenye vichwa vya habari kwa matukio yenye utata

Mwaka 2021, Joe Mfalme na watangazaji wawili waliachishwa kazi katika kituo kimoja cha redio humu nchini baada ya kudaiwa kufanya mzaha dhidi ya mwanamke aliyekuwa katika hatari vya kudhulika.

Muhtasari

• Kwa sasa Joe Mfalme yuko mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa wikendi kwa kudaiwa kuhusika katika mauaji ya afisa wa polisi wa ngazi ya juu.

• Mfalme na wenzake wanatarajiwa kufikishwa mahakamani asubuhi ya leo, Jumatatu Machi 25.

DJ JOE MFALME
DJ JOE MFALME
Image: Facebook

Jina DJ Joe Mfalme, kwa wengi si geni, haswa kwa wanaopenda kuserereka kwenye tafrija na sherehe vilabuni Nairobi.

Mcheza santuri huyo ambaye amejitengenezea jina kwa muda mrefu, kando na kujulikana kwa utendakazi wake mzuri na wa aina yake kwenye mashine za santuri katika hafla mbalimbali, vivyo hivyo katika miaka ya hivi karibuni amekuwa akijipata kwenye vichwa vya habari kutokana na matukio ya utata.

Katika Makala hii, tunaangazia nyakati ambazo Mfalme alijipata kwenye minong’ono ya mitandaoni.

Kukamatwa na polisi akishukiwa kwa mauaji ya afisa wa juu wa polisi

Wikendi iliyopita, DJ Joe Mfalme na timu yake pamoja na maafisa 3 wa polisi walitiwa mbaroni baada ya kushukiwa kuhusika katika mauaji ya afisa wa polisi wa cheo cha inspekta mjini Kikuyu, kaunti ya Kiambu.

Inaarifiwa kwamba Mfalme alizozana na afisa huyo wa polisi wiki moja iliyopita majira ya alfajiri alipokuwa akitoka kazini katika klabu moja mjini Kikuyu. Afisa huyo alidaiwa kukwaruza gari la Mfalme kutoka nyuma kabla ya mzozo kuzuka.

Siku moja baada ya kutiwa mbaroni, Joe Mfalme alivunja kimya chake kupitia taarifa katika kurasa zake mitandaoni.

Katika taarifa yake Jumapili jioni, DJ huyo alisema kuwa yeye na timu yake wamekuwa wakishirikiana vyema na maafisa wa uchunguzi tangu tukio hilo litokee Machi 16, 2024.

"Kwanza kabisa, tunatoa pole kwa familia, marafiki na wote walioguswa na tukio hili la kusikitisha," DJ Joe Mfalme alisema katika taarifa yake.

Aliongeza, “DJ Joe Mfalme na timu yake wamekuwa kwa ushirikiano wa karibu na vyombo vya uchunguzi tangu kutokea kwa tukio hilo. DJ Joe Mfalme na timu yake wamejizatiti kikamilifu kushiriki katika utaratibu wa uchunguzi na wataendelea kutoa ushirikiano wao kadri itakavyohitajika."

Mfalme na wenzake wanatarajiwa kufikishwa mahakamani asubuhi ya leo, Jumatatu Machi 25.

Kuchekwa mitandaoni kwa jibu la utata kwa ujumbe mtamu kutoka kwa mkewe.

Mnamo Desemba mwaka 2022, DJ Joe Mfalme tena alijipata kwenye vichwa vya habari za udaku kufuatia jibu alilotoa kwa ujumbe wenye makopakopa mengi kutoka kwa mkewe.

Mkewe alimwandikia ujumbe mzuri wa kumtakia heri njema siku ya kuzaliwa, lakini jibu ambalo alilitoa liliwaacha wengi kumgeuza kicheko.

“Nimebarikiwa sana kuweza kukuita wangu. Ninakupenda kwa dhati. Wewe ndiye bora zaidi katika ulimwengu huu. Ni kweli. Siwezi kufikiria maisha yangu bila wewe. Heri ya Siku ya Kuzaliwa @djjoemfalme ! Hebu tuifanye kila siku hii kuwa nzuri na Zaburi 91:11 iwe fungu lako; "Kwa maana atawaamuru malaika zake wakulinde katika njia zako zote."

Kwa hili, DJ Joe Mfalme alijibu: “🔥🔥🔥🔥🔥Asante mresh.”

Hata hivyo, katika mahojiano na chombo kimoja cha habari za mitandaoni, Mfalme alitetea jibu lake na kusema kwamba hakuona ubaya wowote kumuita mpenzi wake “mresh”.

Mfalme alisema kwamba yeye na mkewe hawajazoea kuweka mambo yao ya ndoa hadharani kwenye mitandaoni, na hata alijua katika jibu hilo, wengi wangehisi kwamba hampendi lakini ndio hivyo, mambo ya ndoa yake muda wote ni ya faragha.

Kuachishwa kazi redioni kwa matamshi ya mzaha dhidi ya mwanamke aliyekuwa hatarini

Mnamo Machi 2021, DJ Joe Mfalme na wenzake wawili waliachishwa kazi katika kituo kimoja cha redio humu nchini baada ya kudaiwa kutoa matamshi ya kimzaha dhidi ya taarifa za mwanamke aliyekuwa katika hatari ya kudhulika.

DJ Joe Mfalme alikuwa na miezi mitatu tu kwenye tafrija yake mpya kwenye shoo ya asubuhi redioni, pamoja na wenzake wawili, walipoachishwa kazi mwezi Machi kufuatia maoni kuhusu mwanamke mwenye umri wa miaka 20 ambaye aliripotiwa kutupwa kutoka orofa ya 12 ya jengo na mwanamume baada ya kudaiwa kukataa tamaa zake za kushiriki mapenzi.

Siku chache baada ya tukio hilo, Mfalme alitoa taarifa ya kuomba radhi akisema kwamba aligundua kitendo cha kumdhihaki mtu aliye katika hatari ya kudhulika hakikuwa sahihi.

“Natambua kuwa kauli na mchango wangu kuhusu tukio la bahati mbaya lililomtokea Eunice haukuwa sahihi kabisa na unaweza kutafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni wa kutia moyo hasa wakati huu ambao tunatakiwa kusimama kidete kupinga aina yoyote ya Ukatili wa Kijinsia dhidi ya wanawake,” ilisomeka sehemu ya msamaha wake.

Katika mahojiano mengine na Sunday Nation mwaka mmoja baadae baada ya kuachishwa kazi, Joe alisema kwamba alichojifunza ni kutokurupukia mambo na badala yake atakuwa anayafumbia macho ili asije akajipata katika hali sawia.

"Sitajaribu kuwa shujaa tena. Haijalishi hali ninayoona inageuka kuwa mbaya, nitafumbia macho kila wakati,” Mfalme aliiambia Sunday Nation mwaka 2022 Machi.