Post pombe na sherehe wachawi wa kwenu wadhani umepotea – Akothee ashauri

"Acha kupiga Picha mbele ya jasho la watu, wachawi wako wa kijijini watakuendea sana wakidhani umefanikiwa kimaisha. Chapisha pombe na sherehe ili waamini kuwa umepotea," Akothee alishauri.

Muhtasari

• Mama wa watoto watano amekuwa akijionea fahari mjengo huo wa kifahari akishauri watu kutofuata maneno ya watu wa mrengo wa ‘kujenga kijijini ni kuwekeza katika mradi uliokufa’.

AKOTHEE
AKOTHEE
Image: FACEBOOK

Msanii na mjasiriamali Esther Akoth maarufu Akothee amefichua kwamba alianza kufikiria na kuifanya kuwa kweli ndoto yake ya maisha ya kustaafu Zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Akothee kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, alipakia picha za kutoka mwaka 2013 akiwa katika ujenzi wa jumba lake la kifahari, sehemu anayoita makazi yake ya maisha ya ustaafu.

Msanii huyo akitamba kutokana na juhudi zake za kufanikisha ndoto yake kitambo kabla ya wasanii wengine kufikiria kuwekeza katika ndoto kama hiyo, aliwashauri wafuasi wake kwamba kuna muda wa kujivinjari kimaisha na kuna muda wa kufanya kazi.

Akothee alishauri watu kukoma kuwekeza maisha yao katika kujivinjari na kuanza kupiga picha za kutamanisha mbele ya vitu vya kifahari vya watu waliowekeza kutokana na jasho lao halali.

Alisema kwamba hilo litawasaidia kuepuka mitego ya mahasidi wao ambao watadhani ‘wameomoka’ na kuwakazia nati, huku akiwashauri kuonyesha maisha yao ya sherehe mitandaoni ili kuwachanganya mahasidi kudhani kwamba walishapotea kimaisha.

Kuna wakati wa kila jambo, wakati wa kujenga na wakati wa kupiga sherehe. Acha kupiga Picha mbele ya jasho la watu, wachawi wako wa kijijini watakuendea sana wakidhani umefanikiwa kimaisha. Chapisha pombe na sherehe ili waamini kuwa umepotea. Nilijenga nyumba yangu ya kustaafu mnamo 2013, ulikuwa wapi kipindi hicho,” Akothee aliuliza.

Mama wa watoto watano amekuwa akijionea fahari mjengo huo wa kifahari akishauri watu kutofuata maneno ya watu wa mrengo wa ‘kujenga kijijini ni kuwekeza katika mradi uliokufa’.

Miezi kadhaa iliyopita wakati mjadala wa iwapo ni vizuri mtu kujenga kijijini ama kujiendeleza mjini ulipoibuka, Akothee alisimama kidete na kushauri kwamba kujenga ni jambo la muhimu kwani huko ndiko utakapokimbilia na kupaita nyumbani, endapo jambo lolote linakuendea mrama mjini.