"Zoea Bi na Bwana harusi mapema!" Akothee atangaza tukio maalum

Mwimbaji huyo alitangaza Aprili 27, 2024 kuwa siku maalum akidokeza kuwa kuna hafla ambayo itafanyika jijini Mombasa.

Muhtasari

•Akothee amezua mjadala baada ya kushiriki picha yake na meneja wake Nelly Oaks na kuambatanisha na ujumbe wa kimafumbo.

•Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwaomba mashabiki wake wajiandae na kuanza kuzoea Bw na Bi Harusi.

Image: FACEBOOK// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee amezua mjadala baada ya kushiriki picha yake na meneja wake Nelly Oaks na kuambatanisha na ujumbe wa kimafumbo.

Katika chapisho hilo aliloshiriki kwenye Facebook Jumatatu jioni, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwaomba mashabiki wake wajiandae na kuanza kuzoea Bwana na Bi Harusi.

Pia alitangaza Aprili 27, 2024 kama siku maalum akidokeza kuwa kuna hafla ambayo itafanyika jijini Mombasa.

“Zoea Bi na Bwana harusi mapema. Shona kitenge nani wacha panganga. Tukutane tarehe 27 Aprili 2024 katika Klabu ya Gofu ya Nyali Kaunti,” Akothee alitangaza.

Tangazo hilo liliibua hisia mseto kutoka kwa mamia ya mashabiki wake ambao walihisi kuwa huenda alikuwa akidokeza kuhusu kufunga ndoa na meneja wake Nelly Oaks. Hata hivyo, msanii huyo huenda tu anatangaza Mashindano ya Hisani ya Gofu ya Akothee Foundation ambayo yanapangwa kufanyika Mombasa mnamo Aprili 27.

Kwa muda mrefu, Akothee na Nelly Oaks wameaminika kuwa zaidi ya washirika wa kazi tu. Mara nyingi wamedokeza kuhusu kuwa wapenzi.

Takriban miezi minne iliyopita, mama huyo wa watoto watano alionekana kuthibitisha kufufuka kwa mahusiano yake na meneja wake wa muda mrefu Nelly Oaks katika kipindi cha moja kwa moja cha hivi majuzi kwenye mtandao wa TikTok.

Katika kipindi hicho ambacho alikuwa akiwahutubia mashabiki wake Nelly Oaks akimwandalia chakula maalum jikoni, Akothee alisikika akimwita meneja huyo wake ‘babe’ mara kadhaa, jina ambalo hutumika sana sana  wapenzi.

Nelly Oaks pia alisikika akimtaja Akothee kama mtu maalum kwake huku wawili hao wakishiriki matukio ya kimapenzi kwenye kamera.

“Hiki ni chakula cha jioni maalum kwa mtu maalum kama wewe. Ni surprise,” Nelly Oaks alisikika akimwambia mwanamuziki huyo.

Wakati wa kipindi hicho, Akothee kwa hasira aliwasuta wanawake wote waliokiri mapenzi yao kwa meneja huyo wake akidokeza kuwa hapatikani kwao.

Wakati baadhi ya mashabiki walipotaka kujua iwapo Nelly Oaks ana mchumba, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alionekana kuthibitisha kuwa yeye ndiye anashikilia nafasi hiyo.

“Ati kama Nelly ako na mtu?! Kwani mimi mawe? Mimi mawe? Ama mimi ni mti? Unauliza kama Nelly ako na mtu, kwani mimi ni mawe? Ama kijiti? Usinipimie pumzi. Maisha ni ya kwangu nayaendesha vile nataka,” alisema.

Mama huyo wa watoto watano pia alikataa ombi la nambari ya simu ya Nelly Oaks huku akifichua kwamba hata ana uwezo wa kufungua na kutumia simu yake.

“Kweli nikupatie namba ya Nelly? unadhani mimi nimetosheka? Mimi sijarudi soko, mimi ndiye soko, sigawani na mtu,” Akothee alisema.

Nelly Oaks pia aliweka wazi kuwa hapatikani kwa mwanamke mwingine