"Unaifanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi!" Esther Musila asifia mumewe Guardian Angel

Bi Musila ameendelea kuweka wazi mapenzi yake mazito kwa mwanamuziki huyo wa nyimbo za Injili.

Muhtasari

•Bi Musila alichapisha picha za Guardian Angel na kutangaza jinsi  mwimbaji huyo ana uwezo wa kuifanya dunia kuwa mahali pazuri.

•Wawili hao walifunga pingu za maisha mwanzoni mwa mwaka wa 2022 na wamekuwa wakiishi pamoja kwa furaha. 

mnamo siku ya harusi yao Januari 2022.
Esther Musila na mumewe Guardian Angel mnamo siku ya harusi yao Januari 2022.
Image: INSTAGRAM

Mke wa Guardian Angel, Esther Musila ameendelea kuweka wazi mapenzi yake mazito kwa mwanamuziki huyo wa nyimbo za Injili.

Siku ya Jumatatu asubuhi, mama huyo wa watoto watatu alichapisha picha za Guardian Angel kwenye ukurasa wake wa Instagram na kutangaza jinsi  mwimbaji huyo ana uwezo wa kuifanya dunia kuwa mahali pazuri.

Bi Musila alikiri mapenzi yake kwa msanii huyo mwenye umri wa miaka 35 na kueleza kuwa ni miongoni mwa watu wanaoufanya ulimwengu kuwa bora kwa kuwa ndani yake tu.

"Kuna watu fulani ambao hufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri kwa kuwa ndani yake tu. Wewe ni mmoja wao. Nakupenda G wangu,” Bi Musila aliandika kwenye Instagram.

Mama huyo wa watoto watatu wakubwa hajawahi kukwepa kuonyesha waziwazi mapenzi yake kwa mumewe Guardian Angel na kusaidia kipaji chake cha muziki tangu walipoanza kuchumbiana miaka kadhaa iliyopita.

Wakati akizungumza katika mahojiano ya mwezi uliopita na kituo cha habari cha Tanzania, Bi Musila alisifu mapenzi mazito aliyo nayo mume wake Guardian Angel kwake akijigamba kuwa yanamfanya ajihisi mtoto.

Alisema mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 35 anampenda sana bila masharti, jambo ambalo linampa utimilifu mkubwa moyoni mwake.

“Hata bila kumwambia, yeye (Guardian Angel) anajua nampenda sana sana. Kwa sababu amenipa kutimiza maishani mwangu kupita nilivyotarajia,” Esther Musila alisema.

Aliongeza, “Kwa vile ananipenda, kwa vile ananifanyia, yaani nahisi kama mimi ndiye mtoto kwake sasa. Nimeacha kuwa mama kwa umri wangu. Yaani najiskia kama mimi ni mtoto kabisa kwa sababu ya upendo alio nao kwangu.”

Mama  huyo wa watoto watatu wakubwa alibainisha kuwa yeye na Guardian Angel wana urafiki mzuri sana na wenye nguvu ambao unawaunganisha pamoja.

Pia alifichua kuwa tangu walipoamua kufanya maisha pamoja, wanatumia muda wao mwingi pamoja na ni mara chache huwa mbali na kila mmoja.

“Yaani sisi huwa hatuachani, wakati ambao tunaachana ni labda tu nikienda kazini naye aende kazini. Lakini 99% ya maisha yetu huwa tuko pamoja,” alisema.

Aliongeza, “Ningependa tu kumwambia, yaani mpenzi nakupenda tena sana sana. Kutoka kichwani mwangu hadi kidole cha mguu.”

Mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alisema kuwa yeye na mumewe wana muungano mkubwa sana na kusema kwamba wao ni marafiki zaidi kuliko wanandoa.

“Yaani ukipata tuko wawili tu kwa nyumba, tuna utoto, utashangaa hawa ni watoto wagani. Nadhani muungano wetu ni mkubwa, sisi ni marafiki zaidi ya kuwa mume na mke. Ukiniona ninang’ara hivi, yaani ni kupendwa,” alisema.

Aidha, Bi Musila pia alibainisha kuwa katika maisha yake ya zaidi ya miaka 50, hajawahi kuwa na furaha zaidi ya aliyo nayo kwa sasa.

Wawili hao walifunga pingu za maisha mwanzoni mwa mwaka wa 2022 na wamekuwa wakiishi pamoja kwa furaha.