Harmonize kujitosa kwenye pambano la ngumi na bondia maarufu kwa dau la Ksh 13.2M

“Bora nipigwe na mchumba wangu lakini sio wewe Hassan, wewe unafany mzaha na kifo." Harmonize alimwam bia bondia huyo.

Muhtasari

• Harmonize katika tambo zake, alikuwa anasema kwamba alishakula yamini kutomgusa mtu yeyote kwa kumpiga ngumi lakini anataka kutengua nadhiri yake

Harmonize
Harmonize
Image: Insta

Msanii wa kizazi kipya mmiliki wa lebo ya muziki ya Konde Worldwide, Harmonize ametangaza kuuweka muziki pembeni kwa dakika kadhaa na kujitosa kwenye mduara kwa pambano la ngumi.

Msanii huyo alionyesha mazungumzo ya kutambiana na bondia maarufu nchini Tanzania, Hassan Mwakinyo na walionekana kutupiana mikwara kuhusu mchezo wa kupigana ngumi.

Harmonize alikuwa anampa changamoto bondia huyo, akimuambia kwamba kama anajiamini basi akubali kuingia kwenye mviringo, na aliweka wazi kwamba yuko tayari kuwekeza dau la dola laki moja, sawa la shilingi milioni 13.2 pesa za Kenya.

Harmonize katika tambo zake, alikuwa anasema kwamba alishakula yamini kutomgusa mtu yeyote kwa kumpiga ngumi lakini anataka kutengua nadhiri yake japo kwa mara moja tu ili kuzichapa dhidi ya Mwakinyo.

“Bora nipigwe na mchumba wangu lakini sio wewe Hassan, wewe unafany mzaha na kifo. Sijawahi tumia taaluma yangu vibaya, haswa kwa mtu asiyejua moja wala mbili. Sheria haziruhusu kufanya hivyo, lakini hata hivyo, najua wanakuogopa lakini mimi nitakutumia kama mfano.”

“Nilijiapiza kutogusa mwili wa binadamu yeyote, lakini inanibidi kufanya hivyo, mara moja na ya mwisho. Kama una uhakika na unachozungumza, basi tukutane kwenye mduara, dau ni 100k$,” Harmonize alizidisha tambo.

Hata hivyo, Mwakinyo alimwambia kwamba yeye ni msanii mzuri na abaki kwenye njia yake ya muziki, lau sivyo katika masumbwi ataumizwa bure.