Crazy Kennar athibitisha kuanza safari mpya ya masomo Afrika Kusini

Miezi michache iliyopita, mchekeshaji huyo alizua gumzo kwenye mtandao wa X baada ya kudai kwamba bado hajakabidhiwa maua yake na heshimu anayostahili kama mtu mbunifu Zaidi nchini Kenya kuwahi kuhishi.

Muhtasari

• Mchekeshaji huyo ambaye siku za hivi karibuni amekuwa mkimya aliweka wazi kwamba atakuwa anaishi Kenya na Afrika Kusini huku akifanya maudhui ya ucheshi duniani kote.

 
• Safari ya Kennar kwenda kileleni ilianza akiwa bado chuoni. Maudhui yake yalikua kwa kiasi kikubwa huku watumiaji wa mtandao wakiburudika na tabia yake katika ucheshi.

CRAZY KENNAR
CRAZY KENNAR
Image: FACEBOOK

Mchekeshaji Crazy Kennar amethibitisha kwamba kwamba kwa sasa yuko nchini Afrika Kusini ambapo ameamua kujiunga na chuo kimoja kujiendeleza kimasomo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kennar alichapisha picha akiwa jijini Johannesburg kwenye ukuta wa chuo kimoja cha uchumi wa ubunifu na kusema kwamba ndio mwanzo ameianza safari mpya ya kiwango kingine cha burudani.

“Kiwango kipya cha burudani kimefunguliwa, safiri nami ninaposhiriki maisha yangu na wewe kama mbunifu wa Kienyeji wa Kenya anayesoma nchini Afrika Kusini,” Kennar aliandika kwenye picha hizo.

Mchekeshaji huyo ambaye siku za hivi karibuni amekuwa mkimya aliweka wazi kwamba atakuwa anaishi Kenya na Afrika Kusini huku akifanya maudhui ya ucheshi duniani kote.

“Ninaishi nchini Kenya na Afrika Kusini huku nikitengeneza maudhui kote ulimwenguni,” Kennar alisema huku akimalizia kwa ahadi kwa mashabiki wake kwamba watarajie maudhui mengi ya uchekeshaji kibunifu kutoka kwake.

Safari ya Kennar kwenda kileleni ilianza akiwa bado chuoni.

Maudhui yake yalikua kwa kiasi kikubwa huku watumiaji wa mtandao wakiburudika na tabia yake katika ucheshi.

Kupitia maudhui yake, amekutana na watu kadhaa maarufu, akiwemo Trevor Noah ambaye picha yao ya pamoja ameisindika kwenye mwanzo wa picha zake Instagram.

Miezi michache iliyopita, mchekeshaji huyo alizua gumzo kwenye mtandao wa X baada ya kudai kwamba bado hajakabidhiwa maua yake na heshimu anayostahili kama mtu mbunifu Zaidi nchini Kenya kuwahi kuhishi.

Kennar alikwenda mbele na kutoa kidokezo kwa waandishi wa vitabu akiwaambia kwamba ni wakati sasa watunge mswada kumhusu, huku akiwapa mpaka mada ya mswada huo.