KRG aeleza sababu za kufungwa kwa klabu ya Casa Vera Lounge

Msanii huyo hata hivyo alikanusha kwamba kufunguliwa kwa klabu mpya ya Quiver Lounge tawi la Kilimani ndiko kulimaliza Casa Vera kibiashara.

Muhtasari

• Msanii huyo hata hivyo alikanusha kwamba kufunguliwa kwa klabu mpya ya Quiver Lounge tawi la Kilimani ndiko kulimaliza Casa Vera kibiashara.

KRG
KRG
Image: FACEBOOK

KRG the Don, msanii aliyekuwa anatajwa kuwa mmiliki wa klabu ya starehe ya Casa Vera katika mtaa wa kifahari wa Kilimani amefunguka sababu zilizopelekea kufungwa kwa klabu hiyo miezi michache iliyopita.

Miezi miwili iliyopita, KRG alitangaza kufungwa kwa sehemu hiyo ya starehe na sasa anaelezea kilichosababisha biashara yake kupigwa breki.

Akizungumza kwenye Obinna Show Live, KRG alisema kwamba biashara ya burudani jijini Nairobi ni changamoto kiasi akitaja kuwa walevi si wengi jijini bali ni wale wale tu ambao wanazunguka kutoka sehemu moja ya burudani hadi nyingine.

Alisema kwamba iliwabidi kufunga kwa muda ili kupisha ukarabati wa maboresho, akisema kuwa wanahitaji kuboresha ili kuafikia viwango vya sehemu za burudani zinazoshindana na Casa Vera katika utoaji wa huduma za burudani.

“Tumefunga kidogo kwa sababu ya maboresho, unajua vilabu vimefunguliwa vingi katika eneo lile [Kilimani]. Biashara ya klabu ni kama msichana mrembo, kunatokea na wapya kila siku, kwa hiyo kama unampenda lazima utamrudisha saluni kila wakati, kwa hiyo tumerudi katika hatua za mwanzo kidogo kwa sababu pia biashara ya burudani ina changamoto sana kwa kuwa walevi Nairobi si wengi, ni wale tu wanatoka klabu moja kuelekea nyingine,” KRG alisema.

Msanii huyo hata hivyo alikanusha kwamba kufunguliwa kwa klabu mpya ya Quiver Lounge tawi la Kilimani ndiko kulimaliza Casa Vera kibiashara.

KRG alisema kwamba kutokana na ujio wa sehemu nyingi za burudani, iliwabidi kurudi katika hatua za awali kidogo kuangalia mbinu mpya watakazotumia ili kuwashikilia wateja wao pindi watakapofungua tena.

“Sio eti walitufanya tukafunga, ni ushindani ulikuwa juu eneo letu watu walikuwa wamelizoea sana, kwa hiyo ilitubidi tufanye maboresho kidogo,” alieleza.