Mbona watu wanakasirikia mafanikio yangu? Mimi ni bilionea na sio tafadhali - KRG the Don

Msanii huyo mwenye utata amekuwa akijidai kuwa bilionea, jambo ambalo wengi hawajawahi kubali

Muhtasari

• Naendelea kuchanga ndio nifikie akina Elon Mask na matajiri wengine wenye mabilioni ya madola - KRG.

KRG the Don
KRG the Don
Image: Instagram//KRG

Msanii KRG the Don amewacharukia watu ambao wanatilia shaka utajiri wake na thamani yake ya kuwa bilionea.

Msanii huyo kwa mara kadhaa amekuwa akisema kuwa yeye ni tajiri mkubwa ambaye alishapita kiwango cha kuwa milionea na kusema kuwa kwa sasa yeye anaogelea kwenye kiwango kingine cha mabilionea.

Ila wengi wamekuwa wakimpinga vikali huku wakisema thamani yake haijafika hama milioni mia.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, KRG aliwajia juu wale wote wanaoshuku kiwango cha utajiri wake na kusema kuwa yeye ni bilionea na wala hadanganyi.

KRG alisema kuwa haelewi ni kwa nini watu wanaonea wivu utajiri wake na pia kufichua kuwa yumo mbioni kuwekeza mabilioni ili kuwafikia matajiri wengine, akimtaja tajiri namba moja duniani Elon Musk kuwa miongoni mwa watu anaolenga kula nao meza moja ya mabilionea.

Alisema kuwa pesa ambazo anajivunia kuwa nazo si za kupeana kama msaada kwa watu hata kidogo.

Kwanini watu wanakasirikia mafanikio yangu? Niko na Pesa na Sio Tafadhali……….. Na pesa zangu sio za kupea watu bure sababu naendelea kuchanga ndio nifikie akina Elon Mask na matajiri wengine wenye mabilioni ya madola…… Alooooooh! Ni #Bughaaa” KRG alisema.

Wengi wamekuwa wakitilia shaka utajiri wake amabo amekuwa akijidai kumiliki kwa kile amabcho wanasema kuwa katika mafanikio kimuziki, msanii huyo hajatusua sana licha ya kuwepo kwenye tasnia kwa miaka mingi sasa.

KRG ni mmiliki wa sehemu ya kujistarehesha ya Casa Vera iliyopo jijini Nairobi na kando na hiyo, wengi hawajui anamiliki biashara gani zingine za kumzalia mtaji mkubwa mpaka kuwa bilionea.

Je, unaamini KRG ni bilionea ama ni mitikasi tu ya mitandaoni?