(Video) "Unafanya nini na bibi yangu kwa hoteli?" Arrow Bwoy amuuliza KRG baada ya video ya Insta

Arrow Bwoy aliibua swali hilo baada ya KRG kupakia video wakiongozana na Nadia Mukami kutoka kwa hoteli.

Muhtasari

• Baadhi ya mashabiki walihisi huenda ni kiki tu inayotanguliza pengine collabo ya wasanii hao - KRG na Nadia Mukami.

• Wikendi iliyopita Nadia alikuwa na tamasha kubwa mjini Meru, la kwanza tangu achukue likizo ya uzazi.

Msanii kutokea Uganda mwenye makao yake humu nchini, Arrow Bwoy amemchemkia msanii mwenzake KRG the Don kwa kuonekana wakitoka kwenye mgahawa mmoja na mpenzi wake, Nadia Mukami.

Akianzisha malumbano hayo kwenye ukurasa wake wa Instagram, msanii KRG the Don alipakia mkanda wa video ukimuonesha akitoka ndani ya mgahawa huku wameandamana sako kwa bako na msanii wa kike Nadia Mukami ambaye ni mpenzi wa Arrow Bway.

Video ile haikukaa sawa na Arrow Bwoy ambaye moja kwa moja alirusha kombora lake pale huku akitaka kuambiwa sababu ya KRG kuonekana na mkewe katika mgahawa.

“Unafanya nini na bibi yangu kwa hoteli?” Arrow Bwoy aliuliza.

KRG alijipata pagumu kujitetea lakini hatimaye baada ya kujikusanya akapata jibu la kumjibu Arrow Bwoy, na pengine kuzituliza hasira zake.

“Tulia mzee huyu ni sister yangu we just catching up, usianze tena kunitumia goons,” alijibu kwa utani KRG.

Wengi wa mashabiki waliojitoma pale kutoa maoni yao walihisi kabisa hii ni njia moja ya kujitafutia umaarufu huku wakisema huenda msanii Nadia Mukami na KRG wanapika bonge la collabo ambayo wanataka kufukuzia kiki mitandaoni kabla ya kuiachia.

Ikumbukwe wasanii wengi tu humu nchini na nchi Jirani wamekuwa wakifanya mambo mbali mbali kutafuta kiki mradi tu wawe gumzo la mitandaoni kabla ya kuachia ngoma wakiamini kuwa hiyo ndio njia bora ya ngoma kupata mapokezi makubwa na mashabiki.

Nadia Mukami wikendi iliyopita alikuwa na tamasha lake la kukata na shoka mjini Meru, ambalo wachanganuzi wa Sanaa ya burudani wanahisi ni tamasha lililopata mapokezi na mafanikio makubwa, ikizingatiwa kwamba ndio hafla yake ya kwanza kuiandaa tangu achukue likizo fupi ya uzazi.