Kanyari: “Mimi siwezi kuwa maskini kufurahisha watu, nitanunua Helikopta hivi karibuni”

“Kuna watu wengine wanasema Kanyari ni mkora, mimi nimetoka mjengo sasa hivi naendesha V8 zangu, Range Rover… halafu uniambie eti mimi niwe maskini nianze kula githeri na nyama eti ndio nifurahishe watu" alisema.

Muhtasari

• Kanyari alisema licha ya watu kumtukana kwa kuongea na mwanachama wa LGBTQ, Mpenzi Chokuu aliyeko nchini Ujerumani, bado yeye ataendelea kuongea naye, akimtaka kama rafiki yake.

• Hata hivyo, Kanyari alimpa changamoto Chokuu akitaka amfafanulie kauli yake kuwa yeye ni ‘chapati pendua’.

PASTA KANYARI VICTOR
PASTA KANYARI VICTOR
Image: HISANI

Mchungaji wa runingani, Victor Kanyari amefichua kwamba yeye ni mtu ambaye anapenda vitu vizuri katika maisha.

Akizungumza katika moja ya vipindi vyake vya moja kwa moja kwenye mtandao wa TikTok, Kanyari alisema kwamba yeye alipitia maisha ya mateso sana na sasa mahali amefikia hawezi kubali kuwa maskini kwa makusudi ili kuwafurahisha watu.

Kanyari aliwasuta wale wanaomuita mkora akisema kuwa hawezi kuvumilia maisha mabaya ili kufurahisha watu, akisema kuwa yeye ataendelea kuishi maisha mazuri, kula chaula kizuri na hata kuendesha magari ya kifahari kujiburudisha.

Mchungaji huyo alifichua kwamba hivi karibuni, atanunua ndege yake ya kibinafsi aina ya helikopta.

“Kuna watu wengine wanasema Kanyari ni mkora, mimi nimetoka mjengo sasa hivi naendesha V8 zangu, Range Rover… halafu uniambie eti mimi niwe maskini nianze kula githeri na nyama eti ndio nifurahishe watu. Mimi nitakula kuku, nitakula nyama, nitaenda na ndege na hata nitanunua helikopta, haki naapa mbele ya Mungu,” Kanyari alisema.

Mchungaji huyo pia alisema mahali amefika ameyaona mengi na hawezi kukubali kuzama kutokana na presha za watu ambao wanataka wahubiri kuishi maisha Fulani ambayo wanayataka wao.

Kanyari alisema licha ya watu kumtukana kwa kuongea na mwanachama wa LGBTQ, Mpenzi Chokuu aliyeko nchini Ujerumani, bado yeye ataendelea kuongea naye, akimtaka kama rafiki yake.

Hata hivyo, Kanyari alimpa changamoto Chokuu akitaka amfafanulie kauli yake kuwa yeye ni ‘chapati pendua’.

“Ni wahubiri wangapi wamefariki kwa sababu ya presha kutoka kwa watu? Eti watu wanasema Kanyari ni mala*a kisa ninaongea na Chokuu.”

“Chokuu ni rafiki yangu na leo nilikuwa naangalia Instagram yako nikaona wewe ni mtu unapenda kufanya mazoezi ya gym, mimi si mtu wa gym, lakini sasa uliniambia wewe ni chapatti-pendua, sijui hiyo ndio kusema nini. Ulisema wewe ni kwenda mbele kurudi nyuma, nataka kujua hiyo ni nini, na msisahau mimi ni mtumishi wa Mungu aliyepakwa mafuta ya upako wa kipekee,” Kanyari alimaliza kwa tambo.