“Yesu hakufa ili tuwe maskini!” Rose Muhando ajibu wanaokashifu wainjilisti kulipwa kanisani

“Nikuulize, mimi nadaiwa nyumba, nadaiwa karo, nadaiwa kodi mbalimbali za serikali, nilipe na nini wakati kila siku niko njiani kueneza injili? Kwani Yesu alikufa ili sisi tuwe maskini?” aliongeza.

Muhtasari

• Kwa muda, kumekuwa na mjadala mitandaoni kuhusu waeneza injili kupitia nyimbo kutaka kulipwa ili kutumbuiza nyimbo zao kwenye mikutano ya injili inayoandaliwa na wachungaji mbali mbali.

Malkia wa injili katika ukanda wa Afrika Mashariki, Rose Muhando ametoa msimamo wake kuhusu mjadala pevu wa wainjilisti kupewa pesa pindi wanapotokea katika mikutano ya injili kutumbuiza na kuwabariki waumini kwa nyimbo zao.

Akizungumza katika kituo cha redio cha East Africa nchini Tanzania, Muhando anadai kwamba kando na kuwa wainjilisti, pia wao ni binadamu wa kawaida wanaokabiliwa na majukumu ya kila siku ambayo yanahitaji pesa ili kutatuliwa.

Muhando alisema kwamba si haki kwa wainjilisti kuitwa kanisani au kwenye mikutano yoyote ya injili, kuburudisha kwa nyimbo zao kisha kukabidhiwa ‘ahsante ya mdomo’ wakati wana bili nyingi ambazo hazitaki kujua kuwa ni watumishi wa Mungu.

Alisema kwamba hata kwenye maandiko matakatifu, Yesu hakufa msalabani ili watu wake waendelee kuteseka katika umaskini, na ni haki yao pia kupewa ahsante ya pesa pindi wanapotumbuiza kwenye mikutano ya injili.

"Swali langu ni, kazi ni ya Mungu lakini pesa ni za nani? Mungu anasema fedha na dhahabu ni mali yangu. Sasa kile wanachotupa, tunatumia mali ya Mungu kwa ajili ya kazi yake mwenyewe. Kama kazi ni ya Mungu, watambue pia pesa ni za Mungu si zao. Nani aliwahi kusanya sadaka akarusha juu mbinguni zikaenda?” Muhando aliuliza.

“Nikuulize, mimi nadaiwa nyumba, nadaiwa karo, nadaiwa kodi mbalimbali za serikali, nilipe na nini wakati kila siku niko njiani kueneza injili? Kwani Yesu alikufa ili sisi tuwe maskini?” aliongeza.

Kwa muda, kumekuwa na mjadala mitandaoni kuhusu waeneza injili kupitia nyimbo kutaka kulipwa ili kutumbuiza nyimbo zao kwenye mikutano ya injili inayoandaliwa na wachungaji mbali mbali.

Baadhi wamekuwa wakihisi wainjilisti hao wanafaa kutumia kipaji chao walichopewa bure na Mungu kumtumikia yeye katika mikutano ya injili huku wengine wakisema wanastahili kushukuriwa kwa kitu kidogo ili kupata motisha ya kuendelea kueneza injili, na hata kujikimu kimaisha pia.

Maoni yako ni yepi kuhusu wainjilisti kulipwa ili kutumbuiza kwenye hadhara za injili?