Mfahamu Mr Beast: Youtuber mkubwa ulimwenguni

Mr Beast ana jumla ya wafuasi takriban milioni mia mbili sitini na kenda Youtube

Muhtasari

•Ana umaarufu wa kupakia video za maisha ya waja na tamaduni mbalimbali

•Ameangazia ujenzi wa mabwawa ya maji katika bara la Afrika 

Mr Beast kwenye ujenzi wa bwawa
Image: BBC

Jimmy Donaldson almaarufu Mr Beast, ndiye binadamu aliye na wafuasi wengi kwenye ukurasa wake wa kijamii wa YouTube.

Mr Beast, aliye na umaarufu kupindukia ana jumla ya wafuasi takriban milioni mia mbili sitini na kenda akifuatwa na T-series wenye wafuasi milioni mia mbili sitini na sita kwenye ukurasa maarufu wa kimitandao, Youtube.

Mr Beast ana umaarufu wa kupakia video za maisha ya waja na tamaduni mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya ulimwengu ambapo anakuwa na fursa ya kujifunza namna matabaka ya dunia yanastahimili na kuishi kwenye masaibu na suluhu za dunia.

Vilevile Mr Beast ana umaarufu wa kupakia video kwenye mtandao na kisha kuwazawidi wafuasi wake na ruzuku za hela, magari na kadhalika.

Kisa kilicho waacha wengi vinywa wazi ni kile alichokuwa akiwatuza wafuasi wake magari aina ya Tesla akisherehekea siku ya kuzaliwa kwake. Hali hii iliwafanya wengi kusongwa na mawazo jinsi mwanatamasha huyu ana utajiri kupindukia.

Vilevile Jimmy Donaldson amejishirikisha katika kuimarisha ukuaji wa maisha ya watu hasa wanaopitia hali ngumu mfano nchi za Afrika.

Mojawapo ya masuala ambayo Mr Beast ameangazia ni ujenzi wa mabwawa ya maji katika bara la Afrika ambapo amehusisha mataifa kadhaa ikiwemo Kenya, Kamerun, Somalia, Uganda na Zimbabwe katika kandarasi hii adhimu.

Mr Beast alianza shughuli za kupakia video mtandaoni mnamo mwaka wa elfu mbili kumi mbili na kutoka hapo amezidi kupokea umaarufu hatua baada ya nyingine. Yakini mvumilivu hula mbivu vilevile mgagaa na upwa hali wali mkavu.