“Naendelea vizuri!” Chebet athibitisha saa chache baada ya msururu wa jumbe za kutia wasiwasi

Kilichowatia wasiwasi mashabiki wake ni pale alipokiri kwamba katika utafutaji wa amani ya nafsi yake, alijipata amejiingiza kwenye baadhi ya mambo ya kiroho ambayo hawezi kujitoa… mambo ambayo hakuyatarajia.

Muhtasari

• “Kwa wale wanafuatilia, ninaendelea vizuri. Nimefika Nakuru. Nitapokea simu zenu na kujibu jumbe zenu baadae. Ahsante,” Esther Chebet aliandika.

Image: FACEBOOK

Esther Chebet maarufu kama Star Chebet, aliyekuwa muigizaji katika kipindi cha runingani cha The Real Househelps of Kawangware amejitokeza katika mtandao wa Instagram na kuthibitisha kwamba yuko salama na anaendelea vizuri, saa chache baada ya msururu wa jumbe wa kuogofya kuhusu maisha yake.

Muigizaji huyo ambaye wiki chache zilizopita alifichua kuhamia Kericho kutoka Nairobi aliwaacha wengi na maswali ya kusumbua vichwa baada ya kuachia msururu wa jumbe akisimulia kuhusu jambo lililotokea maishani mwake likilenga kumyumbisha.

Baada ya jumbe hizo kuzua taharuki miongoni mwa wafuasi wake, Chebet baadae alirudi na kusema kwamba yuko salama na kuahidi kwamba baadae atapata nafasi ya kupokea simu za wanaomtafuta na pia kujibu jumbe za wanaouliza kuhusu maana kamili ya jumbe zake zenye ukungu mwingi.

“Kwa wale wanafuatilia, ninaendelea vizuri. Nimefika Nakuru. Nitapokea simu zenu na kujibu jumbe zenu baadae. Ahsante,” Esther Chebet aliandika.

Awali, alikuwa amechapisha picha za mto akisema kwamba kuna baadhi ya watu walimhadaa kuondoka Nairobi kwenda Kericho na wakamtumika kufungua portal kwenye mto huo na baadae kujipata ameingizwa kwenye ‘mambo ambayo sikuyatarajia’.

"Nilitumika kufungua portal kwenye mto Kimugu huko Kericho na nikaingizwa kwenye mambo ambayo sikulitarajia. Sikujua ni nini kilikuwa kinatokea hadi kikatokea. Maisha ni ya kiroho na roho huingia kwenye mizozo bila kujua wakati mwingine,” Chebet alisimulia.

“Niko njiani kuelekea Nakuru na gari linasonga.., Hisia zangu zinaonyesha sitakuwa sawa,” aliongeza kwenye sasisho jingine.

Kilichowatia wasiwasi mashabiki wake ni pale alipokiri kwamba katika utafutaji wa amani ya nafsi yake, alijipata amejiingiza kwenye baadhi ya mambo ya kiroho ambayo hawezi kujitoa… mambo ambayo hakuyatarajia.

“…maisha yamekuwa yakienda kasi sana... sijui mwisho wa siku nitakuwa sawa, lakini nilijiingiza kwenye kitu ambacho siwezi kukirudisha nyuma. Maisha ni ya kiroho; Nadhani nilijiingiza kwenye uhalisia usio sahihi katika utafutaji wangu wa amani ya akili na kuingia katika nguvu zisizo sahihi,” alisimulia.