Ujumbe wa Akothee kwa Rais Ruto kuhusu mswada wa fedha

”Wakenya wametawaliwa na dhiki, njaa, hasira na machafuko."

Muhtasari

•Akothee alimueleza Ruto changamto ambazo watoto wakike wanapitia zinazopeleka wengi kuacha shule.

•Akothee pia alimsihi Ruto kufikiria upya mawazo yake kuhusu mswada wa fedha, akiongeza kuwa Wakenya tayari wanateseka na gharama ya juu ya maisha.

Image: FACEBOOK// AKOTHEE

Mwanamuziki na mfanyabiashara Esther Akoth (Akothee) ameshirikiana sababu kwa nini anaamini kwamba mswada wa fedha haufai kupitishwa.

Mama huyo wa watoto watano alitumia Instagram yake kushiriki chapisho refu kwa rais, akitaja athari mbaya ambazo mswada wa fedha utaleta baada ya kuupitisha.

“Mheshimiwa Rais, ni mwaka sasa umepita tangu uchukue wadhifa huo.

Mheshimiwa, wakati unachukua madaraka, presha kwa wananchi ilikuwa tayari imepanda kwa kiwango kikubwa.

Gharama ya maisha imepanda kiasi kwamba wapiga kura wako wengi wanatatizika kumudu milo mitatu kwa siku.

Kama mfadhili, naweza kusema kwa ujasiri kwamba mahitaji ya kimsingi kama taulo za hedhi na mkate ni vitu vya msingi kwa kila mkenya, "alisema.

Aliendelea kueleza rais changamto ambazo wasichana wadogo wanapitia.

Wasichana wadogo wanaacha shule kwa sababu hawawezi kumudu taulo za kujisitiri.

Kwa kukata tamaa, wanalazimika kuuza miili yao kwa mahitaji haya ya kimsingi.

Kutoza ushuru kwa taulo za hedhi ni sawa na kuwaadhibu wanawake kwa mchakato wa asili wa kibaolojia.

Itakuwa afueni kubwa ikiwa taulo za hedhi zingesambazwa bure shuleni.

Kwa sasa, Wakenya wengi hawawezi kumudu hata nguo za ndani, jambo linalowaongezea masaibu.

Akothee pia alimsihi Ruto kufikiria upya mawazo yake kuhusu mswada wa fedha, akiongeza kuwa Wakenya tayari wanateseka na gharama ya juu ya maisha.

”Wakenya wametawaliwa na dhiki, njaa, hasira na machafuko.

 Mheshimiwa nakuomba uangalie upya muswada wa sheria ya fedha na uwasikilize wananchi wako. Kama mkurugenzi wa shule, ninashuhudia wazazi kijijini wakihangaika kupata hata Ksh 300.

Kama mama inaumiza rais tunahitaji mkutano wa kujadili masuala haya. Tafadhali tusikilize sisi wananchi.” Alisema.