“I’m unbwogable!” Larry Madowo ajibu vitisho kisa kusema hajui wanahabari wenza maandamanoni

Siku mbili baadae, Madowo ameonyesha watu kufurika katika DM zake na kumtumia jumbe za matusi na za kumtishia kwa kuwaacha wanahabari chipukizi wa Kenya kudhalilishwa na polisi

Muhtasari

• Hata hivyo, Madowo katika machapisho yake ameonesha ujasiri wake akisema kwamba hayuo tayari kumezeshwa woga.

Image: FACEBOOK

Mwanahabari wa Kenya anayefanya kazi kwenye shirika la habari la kitaifa, CNN Larry Madowo amefichua kwamba baadhi ya watu wameanza kumtishia maisha katika DM zake kwenye mitandao ya kijamii.

Madowo alionyesha baadhi ya jumbe za vitisho kutoka kwa Wakenya ambao walionesha ghadhabu na yeye kutokana na kisa kilichojiri Alhamisi wiki jana wakati wa maandamano jijini Nairobi.

Katika kisa hicho, Madowo alikuwa na makumi ya waandishi wengine wa habari kutoka humu nchini, wengine wakiwa chipukizi ambao walikuwa wanahaha kunasa matukio ya maandamano.

Lakini haikuwa rahisi kwa sababu polisi walikuwa wanazuia baadhi ya matukio kunaswa na watu wasiojulikana kama ni wanahabari.

Katika zogo hilo, polisi walimkabili Madowo na kumtaka kueleza hao aliokuwa nao na Madowo alijibu polisi kwamba hakuwa anawajua bali kila mtu alikuwa akifanya kazi yake kivyake, wala si washirika wake wala wa CNN.

Hili lilipelekea polisi kuwafukuza waandishi hao chipukizi kwa kutojitambua vilivyo.

Tukio hilo lilivutia maoni kinzani katika mitandao ya kijamii, baadhi wakimtuhumu Madowo kwa kushindwa kuwatetea wanahabari wenza huku wengine wakisimama upande wake na kusema kila mmoja alikwenda kunasa matukio ya maandamano kivyake hivyo haikuwa lazima Madowo kuwatetea kwa polisi.

Siku mbili baadae, Madowo ameonyesha watu kufurika katika DM zake na kumtumia jumbe za matusi na za kumtishia kwa kuwaacha wanahabari chipukizi wa Kenya kudhalilishwa na polisi wakati wa maandamano badala ya kuwatetea.

Hata hivyo, Madowo katika machapisho yake ameonesha ujasiri wake akisema kwamba hayuo tayari kumezeshwa woga.

“Mimi ni unbwogable,” Madowo alisema katika moja ya chapisho lake Facebook.