“Silaumu mtu yeyote ni pombe nakunywa sana” – Magix Enga baada ya kugonjeka aki’shoot video

“Nimejaribu kufurahi leo nikijaribu kushoot video ya muziki lakini siku imeniendea vibaya nakohoa damu stay safe siwezi kumlaumu mtu ni pombe nakunywa sana God atanisaidia,” Magix Enga aliandika.

Muhtasari

• Enga alidokeza kwamba alijipata katika hali ya kutishia uhai wake wakati alipokuwa akiandaa video ya wimbo wake mpya na ghafla afya ya mwili wake ikamsaliti na kuanza kutabika damu.

Magix Enga
Magix Enga
Image: Facebook,

Produsa matata wa humu nchini Magix Enga amedokeza kuwa bado anazidi kupambana na jinamizi la uraibu na utiribu wa mtindi.

Hii ni licha ya marafiki kuungana pamoja na kumsaidia kaitka mchakato wa kuvunja ndoa yake na pombe na hata kumhamisha hadi mjini Eldoret kwa ajili ya kuendeleza kazi yake ya kuzalisha miziki kwa wasanii.

Produsa huyo ambaye pia ni msanii kupitia ukurasa wake wa Facebook sasa anadokeza kwamba vita yake dhidi ya ulevi vina changamoto si haba, akisema kwamba hawezi mlaumu mtu yeyote kwa masaibu yake.

Enga alidokeza kwamba alijipata katika hali ya kutishia uhai wake wakati alipokuwa akiandaa video ya wimbo wake mpya na ghafla afya ya mwili wake ikamsaliti na kuanza kutabika damu.

Hata hivyo, alisema kwamba hali hiyo si ya kulaumiwa kwa mtu yeyote yule, akikiri kwamba ni kutokana na matumizi ya pombe kupita kiasi na hata kusema kwamba anatumai Mungu atamng’atua kutokana na uraibu huo.

“Nimejaribu kufurahi leo nikijaribu kushoot video ya muziki lakini siku imeniendea vibaya nakohoa damu stay safe siwezi kumlaumu mtu ni pombe nakunywa sana God atanisaidia,” Magix Enga aliandika.

Hata hivyo, katika sasisho lingine, Enga alisema kwamba mke wake amekuwa mmoja wa watu wanaokaa karibu naye katika changamoto hizo na kumshukuru kwa mapenzi ya kweli baina ya uraibu wake.

“Naweza kusema mke wangu ndiye bora, Mungu akubariki. Wakati mwingine ukiwa mgonjwa sana unahitaji mtu wa kuzungumza naye. Na wangu ameni save siku mingi that's what we call love. Kwa shida na raha. Mama Starboy,” alisema.

Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa produsa huyo aliyejizolea umaarufu kwa midundo yake ya miziki ya Gengetone, kuzungumzia jinsi suala la uraibu wa pombe limemtia mavumbini.