Shakib ajuta kuhusu kauli chungu alizotoa kumhusu Zari, adai zilichangiwa na hasira

"Nilisema mengi kwa hasira. Haikusudiwa kuwa hivyo. Sikujua nilikuwa nikirekodiwa. Ingawa nilikuwa na hasira, kuna mambo ambayo singezungumza,” Shakib aliongeza kwa majuto.

Muhtasari

• Majuto ya Shakib yanakuja siku chache tu baada ya Zari pia kuomba radhi kwa Shakib, akikiri kuwa mlipuko wake kwenye mitandao ya kijamii ulitokana na kuchanganyikiwa.

• Alifafanua kuwa safari yake ya hivi majuzi mjini Kampala ilikusudiwa kurudiana na mumewe, akikiri kuwa kujitangaza mtandaoni ni kosa.

ZARI NA SHAKIB
ZARI NA SHAKIB
Image: Instagram

Mfanyibiashara Shakib Cham Lutaya amefunguka kwa majuto makubwa kuhusu kauli za uchachu alizozitoa kumhusu mpenzi wake, Zari Hassan wiki kadhaa zilizopita.

Shakib alisema kwamba kauli hizo hazikuonyesha picha yake halisi bali zilikuwa zimegubikwa na hasira baada ya kumuona Zari akila bata na Ex wake, Diamond Platnumz.

Lutaya alifichua kuwa mazungumzo ya faragha ambayo alitoa kauli kali dhidi ya Zari yalirekodiwa kwa siri na kuvujishwa na rafiki yake wa karibu.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Shakib alieleza: “Sikutoa sauti. Rafiki yangu alinipigia simu baada tu ya video ya moja kwa moja ya Zari kusambaa, na bado nilikuwa nimekasirika. Niliathiriwa sana na kile nilichokiona.”

“Sina marafiki wengi wanaoniangalia, na walipopiga simu, nilisema mengi kwa hasira. Haikusudiwa kuwa hivyo. Sikujua nilikuwa nikirekodiwa. Ingawa nilikuwa na hasira, kuna mambo ambayo singezungumza,” Shakib aliongeza kwa majuto.

Majuto ya Shakib yanakuja siku chache tu baada ya Zari pia kuomba radhi kwa Shakib, akikiri kuwa mlipuko wake kwenye mitandao ya kijamii ulitokana na kuchanganyikiwa.

Alifafanua kuwa safari yake ya hivi majuzi mjini Kampala ilikusudiwa kurudiana na mumewe, akikiri kuwa kujitangaza mtandaoni ni kosa.

Zari alikiri aliruhusu hisia zake kumshinda na kutumia "jukwaa lisilo sahihi" kuelezea hisia zake.

Mnamo Agosti, Zari alikuwa ametumia mtandao wa kijamii kumkumbusha mumewe, Shakib Lutaaya, juu ya jukumu lake dogo maishani mwake, akimtaka kuwa mwangalifu katika uhusiano wao.

Kuchanganyikiwa kwake kulizuka pale Shakib alipoonyesha kutofurahishwa na ukaribishaji wake Diamond Platnumz, baba wa watoto wake.

Diamond alikuwa amesafiri kwenda Afrika Kusini kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa kwa Tifah, binti anayeishi na Zari.