"Sina kitu!" Nyota Ndogo alalamika baada ya kutajwa msanii namba 2 kwa utajiri Mombasa

Alilalamika kuwa wanaomuorodhesha miongoni mwa wasanii tajiri wanamweka katika hatari ya kuibiwa.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili alishangaa vigezo vilivyotumika kubaini wasanii tajiri zaidi katika kaunti hiyo.

•Aliwataka watafiti kutoangazia utajiri wa mume wake wa mzungu Henning Nielsen wanapoangalia thamani yake.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwimbaji mkongwe Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo ameibua malalamishi baada ya kuorodheshwa nambari mbili kwa wasanii matajiri zaidi Mombasa.

Akizungumza kwenye video aliyochapisha Instagram, mama huyo wa watoto wawili alishangaa vigezo vilivyotumika kubaini wasanii tajiri zaidi katika kaunti hiyo.

Nyota Ndogo alidokeza kuwa hakuba pesa za kutosha katika akaunti yake kumfanya awe  kileleni mwa orodha.

"Nimewekwa namba mbili kwa wasanii matajiri Mombasa. Huu utafiti wao wanaufanyaje? Maana benki yangu ipo tupu," alisema.

Mwanamuziki huyo mzaliwa wa Pwani aliweka wazi kwamba pia yeye anahangaika kutafuta pesa za kukidhi mahitaji yake. Alibainisha kuwa yeye ni mwanamke wa kawaida tu anayefanya biashara ya hoteli katika mji wa Voi.

Aidha, alilalamika kuwa watafiti wanaomuorodhesha miongoni mwa wasanii tajiri  wanamweka tu katika hatari ya kuibiwa.

"Huo utajiri sijui umekuja vipi. Jamani, ndio wale majambazi wakishasoma naanza kuandamwa. Nafuatwa ni mie hata gari kutia mafuta ni balaa. Mimi hata kwenye orodha msiniweke maana mimi ni wa kawaida," alisema.

Aliwabainishia majambazi ambao wamekuwa wakimfuatilia kuwa hana chochote cha kuibiwa.

"Mimi ni mama nitilie, huo utajiri sijui unatoka wapi. Tuambie mwajuaje sisi matajiri," alisema.

Nyota Ndogo alisisitiza kwamba imekuwa muda mrefu tangu alipoachia muziki wake wa mwisho. Kufuatia hilo, alipendekeza kwamba jina lake linafaa kuwekwa katika orodha ya wafanyibiashara wa hoteli. 

"Mimi mngeniweka katika orodha ya wasanii wanaojitahidi. Wasanii ambao wanajituma kwa mambo mengine ili kupata chakula na karo ya shule.. Maanake mimi najitahidi. Lakini kwenye utajiri nifuteni," alisema.

Pia aliwataka watafiti kutoangazia utajiri wa mume wake wa mzungu Henning Nielsen wanapoangalia thamani yake.

"Muwekeni kando huyo mzungu. Mimi ata huwa najihesabu kama hayuko," alisema.

Aliweka wazi kwamba huwa anajituma zaidi bila kumtegemea mumewe ili itokeapo watengane basi asiachwe akihangaika.