"Tafadhali mponye binti yangu!" Diana Marua amlilia Mungu baada ya bintiye kulazwa siku tano

Mkewe Bahati ametoa taarifa kuhusu afya ya mtoto wao mdogo baada ya kulazwa hospitalini.

Muhtasari

•Siku ya Jumamosi, mke huyo wa Bahati alionyesha picha kadhaa za binti huyo wa miezi mitano akihudumiwa na wahudumu wa afya.

•Diana alioa shukrani kwa wahudumu wa afya ambao wamekuwa wakimshughulikia mtoto huyo wake wa mwisho.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu Diana Marua amethibitisha kuwa bintiye mdogo, Malaika Bahati amelazwa katika hospitali kwa siku tano zilizopita.

Siku ya Jumamosi, mke huyo wa Bahati alionyesha picha kadhaa za binti huyo wa miezi mitano akihudumiwa na wahudumu wa afya.

"Siku ya 5, Mtoto wangu Malaika Bahati, afya njema ni sehemu yako kwa jina la Yesu," aliandika chini ya picha alizopakia Instagram.

Pichani, mama huyo wa watoto watatu alionekana akiwa amemshika bintiye huku akimpa maziwa kwa chupa.

Aliendelea kutoa shukrani kwa wahudumu wa afya ambao wamekuwa wakimshughulikia mtoto huyo wake wa mwisho.

"Wanafanya kila kitu kuhakikisha Laika anakuwa vizuri na anapata nafuu. Mungu naomba umponye binti yangu," alisema.

Mumewe, Bahati pia alichukua fursa hiyo kumtakia afueni mtoto huyo wao wa miezi mitano.

Mwimbaji Bahati alikuwa wa kwanza kufichua kwamba  binti yake Malaika Bahati ni mgonjwa siku chache zilizopita..

Siku ya Alhamisi, baba huyo wa watoto wanne alisema  bintiye huyo wa miezi mitano amelazwa  hospitalini tangu mapema wiki hii.

"Baby Malaika amelazwa katika Hospitali ya Komarock Modern kwa siku 3 zilizopita na tunamuombea Malaika apone haraka," Bahati alisema katika taarifa fupi kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mwanamuziki huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akiwa amemshika Malaika huku muuguzi mwanamke akimhudumia.

Aliendelea kumuombea mtoto huyo wake mdogo afueni ya haraka.

"Uponyaji wa Mungu uwe juu yako binti yangu Malaika Bahati," alisema.

Taarifa nyingine iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Baby Malaika iliashiria kwamba alikuwa anaendelea kupata afueni  hospitalini.

"Nimekumbatiwa kwa upendo na utunzaji. Ninaendelea vizuri hapa hospitalini," ilisema taarifa hiyo.

Picha ya Diana Marua akiwa amemkumbatia mtoto huyo wake iliambatana na taarifa hiyo ya siku ya Alhamisi.

Malaika Bahati, ambaye ni mtoto wa tatu wa Bahati na Diana Marua alizaliwa mnamo Novemba mosi mwaka jana.

Baada ya Diana kujifungua, Bahati alimpongeza na kumshukuru kwa kuwa mzazi wa watoto wake na zaidi kuwa mama bora.

"Nimekupenda zaidi kwa kubeba ujauzito na kulea watoto wangu.... ILA Nimekuheshimu ZAIDI kwa kujiamini katika chumba cha upasuaji ulipopitia upasuaji  wa kumkaribisha Binti Yetu @MALAIKA_BAHATI," alisema.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili wa zamani alisema  alishuhudia jinsi mkewe alivyokuwa mtulivu wakati wa upasuaji wa kujifungua (CS)  na kueleza jinsi alivyomthamini na kumheshimu kwa yote hayo.