Binti mdogo wa Bahati na Diana Marua alazwa hospitalini baada ya kuugua

"Uponyaji wa Mungu uwe juu yako binti yangu Malaika Bahati," Bahati aliomba.

Muhtasari

•Siku ya Alhamisi, Bahati alisema  bintiye huyo wa miezi mitano amelazwa  hospitalini tangu mapema wiki hii.

•Taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Baby Malaika iliashiria kuwa anaendelea kupata afueni  hospitalini.

Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za mapenzi Kelvin Kioko almaarufu Bahati amefichua kwamba bintiye  mdogo, Malaika Bahati ni mgonjwa.

Siku ya Alhamisi, baba huyo wa watoto wanne alisema  bintiye huyo wa miezi mitano amelazwa  hospitalini tangu mapema wiki hii.

"Baby Malaika amelazwa katika Hospitali ya Komarock Modern kwa siku 3 zilizopita na tunamuombea Malaika apone haraka," Bahati alisema katika taarifa fupi kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mwanamuziki huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akiwa amemshika Malaika huku muuguzi mwanamke akimhudumia.

Aliendelea kumuombea mtoto huyo wake mdogo afueni ya haraka.

"Uponyaji wa Mungu uwe juu yako binti yangu Malaika Bahati," alisema.

Taarifa nyingine iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Baby Malaika iliashiria kuwa anaendelea kupata afueni  hospitalini.

"Nimekumbatiwa kwa upendo na utunzaji. Ninaendelea vizuri hapa hospitalini," ilisema taarifa hiyo.

Picha ya Diana Marua akiwa amemkumbatia mtoto huyo wake iliambatana na taarifa hiyo ya siku ya Alhamisi.

Malaika Bahati, ambaye ni mtoto wa tatu wa Bahati na Diana Marua alizaliwa mnamo Novemba mosi mwaka jana.

Baada ya Diana kujifungua, Bahati alimpongeza na kumshukuru kwa kuwa mzazi wa watoto wake na zaidi kuwa mama bora.

"Nimekupenda zaidi kwa kubeba ujauzito na kulea watoto wangu.... ILA Nimekuheshimu ZAIDI kwa kujiamini katika chumba cha upasuaji ulipopitia upasuaji  wa kumkaribisha Binti Yetu @MALAIKA_BAHATI," alisema.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili wa zamani alisema  alishuhudia jinsi mkewe alivyokuwa mtulivu wakati wa upasuaji wa kujifungua (CS)  na kueleza jinsi alivyomthamini na kumheshimu kwa yote hayo.

"Kwa uhakika siwezi kukufananisha na mwanamke yeyote chini ya jua... Kwa sababu hakuna anayejua ulipitia nini ili niweze kuitwa baba tena!!! Hakika Wewe ni  Super Woman wangu, mama @MALAIKA_BAHATI ," Alisema Bahati.

Wanandoa hao wana watoto wengine wawili pamoja, Heaven Bahati na Majesty Bahati. Pia wanamlea mvulana wa miaka 13, Morgan Bahati ambaye mwanamuziki huyo alimchukua kuwa wake miaka kadhaa iliyopita.

Bahati ana binti mwingine na mpenzi wake wa zamani, Yvette Obura.