"Mezeni kiwaru" Diana awatupia vijembe wapenzi wa zamani huku akifurahia mahaba ya Bahati

"Sasa ma'Ex wetu wanasikiangaje jamani?? Huku ni mahaba tu," Diana alihoji.

Muhtasari

•Diana alishangaa jinsi wapenzi wao wa zamani huwa wanahisi kila wanapowaona wakiwa na furaha pamoja.

•Diana Marua alimhakikisha mume wake Bahati kwamba moyo wake tayari umekwama kwake na hatoki ng'o.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu na mwimbaji maarufu Diana Marua amewatupia vijembe wapenzi wake wa zamani ambao walichoka naye na kumtema.

Siku ya Jumamosi, mke huyo wa mwimbaji wa nyimbo za mapenzi Kelvin Kioko almaarufu Bahati alishangaa jinsi wapenzi wao wa zamani huwa wanahisi kila wanapowaona wakiwa na furaha pamoja.

"Sasa ma'Ex wetu wanasikiangaje jamani?? Huku ni mahaba tu," Diana Marua alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa watoto watatu aliwataka wale waliokata tamaa naye katika mahusiano yake ya awali kuendelea kumuonea gere.

"Wenye waliniacha mezeni kiwaru," alisema.

Wakati huo huo, Diana Marua alimhakikisha mume wake Bahati kwamba moyo wake tayari umekwama kwake na hatoki ng'o.

"Nishatulia kwako kipenzi. Nishakuwa asali, nilambe polepole." Diana alimwambia mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili.

Bahati kwa upande wake alitumia maneno ya wimbo wa Harmonize 'Nitaubeba' kumsifu mkewe na kubainisha jinsi walivyoridhika  na mahusiano yao.

"Siku hizi mbona sikuskii tena, sikuskii ukilia, sikuskii ukisema.. Niko busy na Boo jamani nimeshasema. Bize na mpenzi @diana_marua," alisema.

Wanandoa hao ambao wamekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka sita sasa walikuwa Dubai hivi majuzi ambapo walipata kazi kubwa ya ubalozi.

Mapema mwezi Februari, Diana Marua aliadhimisha miaka saba ya kuwa pamoja na bosi huyo wa Eastlands Most Beloved Records (EMB) .

Katika chapisho la Instagram, mama huyo wa watoto watatu alionyesha fahari yake kuona jinsi wanavyofanana sana.

Alibainisha kuwa yeye na Bahati wanafanana sio kimuonekano tu bali pia, kimavazi na hata lugha yao ni sawa.

"Miaka 7 ambayo imepita, tunafanana 😂, tunaongea lugha moja, vicheko vyetu ni vinafanana na tangu wakati wote hatujawahi kuacha kufananisha mavazi yetu 💃," aliandika chini ya picha zake na mumewe wakiwa na mavazi sawa.

Mwanavlogu huyo alidokeza kuwa mapenzi yake na mwimbaji huyo wa zamani wa injili ni ya kweli na ya kujivunia.

Bahati kwa upande wake alibainisha kuwa maisha yake yalikamilika wakati ambapo alimpata mke huyo wake na kuweka wazi kuwa amemtosha.

"Nilipokupata, nilipata nusu yangu bora na unatosha Diana Marua," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Bahati alimtambulisha Diana kama 'mshirika wake wa maombi' takriban miaka sita iliyopita kabla ya kubainika kuwa wanachumbiana.

Wawili hao wamekuwa wakiishi pamoja katika ndoa na tayari wamebarikiwa na watoto watatu pamoja. Pia wanalea mtoto mwingine mmoja, Morgan Bahati ambay Bahati alitoa kwenye chumba cha watoto.

Mwaka jana, Bahati alifunguka kuhusu mipango ya kufunga pingu za maisha na Diana Marua hivi karibuni.

Katika sherehe ya kufichua jinsia ya mtoto, mwanamuziki huyo alisema kuwa anapanga harusi kubwa ya kifahari.

Alisema sababu ya kukawia kufanya harusi licha ya kuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu ni kwa kuwa hangetaka kufanya harusi ndogo.

"Unajua mimi ni mtu anayependa kufanya mambo kwa kuongeza ladha, nikiandaa hafla napenda kuandaa hafla kubwa," alisema.

Kabla ya kujitosa kwenye mahusiano na Diana Marua, mwimbaji huyo alikuwa akichumbiana na Yvette Obura ambaye ana binti mmoja naye.