Mpenzi wa DJ Fatxo aeleza sababu ya kusimama naye licha ya kuhusishwa na mauaji ya Jeff Mwathi

Gathoni alimtia moyo mpenziwe na kumuomba awe na ujasiri wakati matokeo ya uchunguzi yakisubiriwa.

Muhtasari

•Gathoni alisema mwimbaji huyo wa Mugithi ana maana kubwa kwake na kuweka wazi kuwa hayuko tayari kuacha kumpenda.

•Gathoni alibainisha kuwa yeye na mpenziwe wameweza kutimiza malengo mengi katika kipindi kifupi ambacho wamekuwa pamoja.

DJ Fatxo na Mpenziwe
Image: INSTAGRAM// GATHONI WARUGURU

Huku uchunguzi wa mauaji ya Jeff Mwathi ukiwa umeingia katika hatua za mwisho mwisho, anayeaminika kuwa mpenzi wa  DJ Fatxo, Gathoni Waruguru amemtia moyo mwimbaji huyo wa Mugithi na kukiri mahaba mazito kwake.

Katika taarifa yake ya Jumamosi jioni, Gathoni ambaye ni mtangazaji katika kituo cha habari cha Kikuyu alikanusha madai ya kuwa na upendeleo na kusisitiza kuwa anasimama na mpenzi wake kwa sababu anampenda sana.

Alisema mwimbaji huyo wa Mugithi ana maana kubwa kwake na kuweka wazi kuwa hayuko tayari kuacha kumpenda.

"Mimi sio mwandishi wa habari mwenye upendeleo, mimi ni "msichana wa kijijini" ambaye yuko katika mapenzi (Huwa naweka viapo kwa taarifa yenu) ," Gathoni alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mtangazaji huyo wa habari alishangaa kwa nini alibahatika kupata DJ Fatxo kama mpenzi wake huku akibainisha ni ndoto yake iliyotimia.

"Tangu uingie kwenye maisha yangu, nimekuwa nikipaa katika Cloud 9 na sijashuka bado. Bado sijajua nilichofanya kuwa na bahati ya kuwa na wewe katika maisha yangu, ndoto yangu ilitimia. Ninashukuru sana kwa hilo," alisema.

Gathoni alibainisha kuwa yeye na mpenziwe wameweza kutimiza malengo mengi katika kipindi kifupi ambacho wamekuwa pamoja.

"Siwezi kusubiri kuona yaliyo mbele katika siku zetu za usoni. Mungu Kwanza," alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mtangazaji huyo kumwandikia DJ Fatxo maneno mazuri ya kumtia moyo huku uchunguzi wa kifo cha Jeff Mwathi ambaye aliaga dunia nyumbani kwake mwezi Februari  ukielekea kukamilika.

Gathoni alitumia maneno ya Biblia kumtia moyo mpenzi huyo wake na kumuomba awe na ujasiri huku matokeo ya uchunguzi yakisubiriwa.

"Basi usiogope, kwa maana mimi niko  pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu na kukusaidia. Nitakushika kwa mkono wa haki yangu." aliandika kwenye Instagram siku ya Alhamisi.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha yake na mcheza santuri huyo.

"Unaweza kukabiliana na haya!" alimwambia.

Mwimbaji DJ Fatxo, binamu yake pamoja na marafiki wengine ambao walikuwa na Jeff wakati wa kifo chake mnamo Februari 22, mwaka huu wametajwa kama baadhi ya watu wa kuangaziwa katika kesi hiyo.