Sampuli za DNA za DJ Fatxo, wenzake zachukuliwa kubaini ikiwa Jeff Mwathi alidhulumiwa kingono

DCI walisema kuwa tayari wamefanya sehemu kubwa ya uchunguzi wa kesi hiyo.

Muhtasari

•DCI walisema kwamba sampuli za DNA za Jeff Mwathi pamoja na wahusika muhimu katika kesi hiyo pia zilichukuliwa.

•Wapelelezi walitoa ombi kwa wanafamilia na Wakenya wote kwa jumla kuwa na subira wanapokamilisha uchunguzi wao.

Marehemu Jeff Mwathi na DJ Fatxo
Image: HISANI

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imetoa taarifa kuhusu uchunguzi unaoendelea wa kifo cha marehemu Geoffrey 'Jeff' Mwathi.

Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin aliagiza wapelelezi wake kuanzisha upya uchunguzi wa kifo cha kijana huyo wa miaka 23 mapema mwezi uliopita kufuatia agizo kuu la waziri wa masuala ya ndani, Kindiki Kithure.

Katika taarifa ya siku ya Alhamisi, Idara hiyo ya upelelezi iliweka wazi kuwa tayari wamefanya sehemu kubwa ya uchunguzi wa kesi hiyo iliyoangaziwa kote nchini na sasa wako katika hatua za mwisho mwisho.

"Kufikia sasa, timu ya kuchunguza mauaji na wataalam wa Maeneo ya Uhalifu walio katika Maabara ya Kitaifa ya Uchunguzi wa Kitaifa ya DCI wametembelea tena eneo la tukio, walifanya zoezi la kisayansi la ujenzi wa eneo la tukio na kurekodi taarifa mpya kutoka kwa mashahidi katika nia ya kutegua fumbo la kifo

Kufikia sasa, kutokana na mapendekezo ya wataalamu wa Mauaji, mwili wa marehemu umefukuliwa kwa uchunguzi mpya, na sampuli  zimechukuliwa ili kubaini kama  alikunywa pombe kabla ya tukio na kubaini asilimia yake, au sumu nyingine yoyote ilitumiwa kabla ya kifo chake," DCI walisema katika taarifa.

Wapelelezi walisema kwamba sampuli za DNA za Jeff Mwathi pamoja na wahusika muhimu katika kesi hiyo pia zilichukuliwa ili kubaini ikiwa marehemu alinyanyaswa kingono kabla ya kifo chake mnamo Februari 22.

Picha za CCTV pia zimechukuliwa kutoka kwa nyumba ya DJ Fatxo ambako marehemu alikuwa alipokumbana na kifo chake.

"Wakati huo huo, kwa sasa tunasubiri ripoti kutoka kwa mwanapathojia wa serikali, ambayo itatujulisha sehemu ya hatua yetu ya mwisho," DCI walisema.

Aidha, wapelelezi walitoa ombi kwa wanafamilia na Wakenya wote kwa jumla kuwa na subira wanapokamilisha uchunguzi wao.

Mwimbaji wa Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo, binamu yake pamoja na marafiki wengine ambao walikuwa na Jeff wakati wa kifo chake wametajwa kama baadhi ya watu wa kuangaziwa katika kesi hiyo.