DCI wakusanya sampuli zaidi kubaini kama Jeff Mwathi alilawitiwa kabla ya kuuawa!

"Tumechukua sampuli kutoka eneo la haja kubwa ambazo zitafanyiwa DNA" mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor alisema.

Muhtasari

• Hata hivyo, Oduor alisema kwamba uchunguzi wa pili haukutofautiana na wa awali kwamba Mwathi alifariki kutokana na majeraha mabaya ya kichwa.

Jeff Mwathi, aliyefariki kwa utata nyumbani kwa DJ Fatxo
Jeff Mwathi, aliyefariki kwa utata nyumbani kwa DJ Fatxo
Image: Facebook//Simon Mwangi Muthiora

Mapema Ijumaa wachunguzi kutoka idara ya upelelezi ya DCI, kitengo cha kuchunguza maafa ya utata ya nyumbani walifika katika boma la wazazi wa marehemu Jeff Mwathi wakiongozana na mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor Kwa lengo la kuufukua mwili wa mbunifu huyo wa mitindo ili kuzamia Zaidi kiini cha kifo chake.

Sasa imebainika kuwa sehemu ya uchunguzi huo ilikuwa ni kukusanya sampuli Zaidi ili kubaini ukweli nyuma ya kifo cha utata mwingi cha Mwathi, ikiwemo kutegua dhana kwamba huenda alilawitiwa kabla ya kuuawa.

Wiki mbili zilizopita baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa awamu ya kwanza, DCI walibaini kwamba Mwathi hakujituoa kutoka ghorofani kama ilivyorekodiwa katika ripoti, bali aliuawa.

Mwanapatholojia Mkuu wa Serikali Johansen Oduor, aliyefanya uchunguzi wa pili baada ya mwili huo kufukuliwa huko Njoro, Kaunti ya Nakuru, alifichua kuwa sampuli zilichukuliwa ili kubaini ikiwa Mwathi alilawitiwa au la.

“Kumbuka kulikuwa na tuhuma za kulawiti; tumechukua baadhi ya sampuli ambazo zitatusaidia kujua ukweli uliosababisha kifo cha Jeff,” alisema.

"Tumechukua sampuli kutoka eneo la haja kubwa ambazo zitafanyiwa DNA. Tumechukua sampuli kwa ajili ya uchambuzi wa sumu ili kujua kama baadhi ya sumu zilihusika au dawa kwa hivyo sasa tutachambua na kupata matokeo.

Maafisa wa upelelezi pia walipima upana wa kifua cha Mwathi ili kubaini ikiwa aliruka kutoka kwenye ghorofa kupitia dirishani kama ilivyodaiwa wakati wa uchunguzi wa awali.

Bw. Oduor aliendelea kufichua kuwa uchunguzi wa pili wa maiti uliofanyika Ijumaa haukufichua tofauti zozote na wa kwanza, akiongeza kuwa Mwathi alifariki kwa majeraha mabaya kichwani.