Willy Paul afunguka kwa nini hajakuwa akitoa muziki siku za hivi majuzi

Pozee alitumia fursa hiyo kuwashambulia wanamuziki wenzake Wakenya akudai wamejaribu kuachia muziki lakini hakuna matokeo.

Muhtasari

•Willy Paul alidai kuwa alisitisha kutoa nyimbo mpya ili kuwaonyesha watu jinsi tasnia ya muziki ya Kenya ilivyo duni bila yeye.

•Wimbo wa mwisho ambao Willy Paul alitoa wenye video ni ‘POPO’ ambao alimshirikisha Miss P Aprili mwaka huu.

Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Mwanamuziki wa Kenya Wilson Radido almaarufu Willy Paul ameweka wazi kuwa amekuwa hatoi muziki mpya katika siku za hivi majuzi kwa makusudi .

Katika taarifa yake ya Alhamisi asubuhi, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alidai kuwa alisitisha kutoa nyimbo mpya ili kuwaonyesha watu jinsi tasnia ya muziki ya Kenya ilivyo duni bila yeye.

Pozze alidai kuwa wakati wa mapumziko yake ya kuachia muziki, wanamuziki wenzake wengi wamefanya nyimbo mpya lakini hawajawaridhisha mashabiki.

“Pole sana familia, najua nimewavunja mioyo wengi wenu kwa kutotoa Muziki Mpya. Kwa kweli, nilifanya hayo yote kwa kusudi ili Kuwaonyesha Nyote Jinsi Tasnia Inavyo mbaya bila pembejeo langu. Wengine Watatofautiana Na Mimi Lakini Wengi Wataegemea Upande Wangu. Wanamuziki Wamejaribu Kutoa maudhui lakini Waaaaapppi??,” Willy Paul alisema kupitia Instagram.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Umeme’ hata hivyo alitangaza kuwa sasa atamaliza mapumziko yake na akaahidi kuachia wimbo mpya hivi karibuni.

“Nimefurahi Sasa Kila Mtu Anafahamu Kwamba Bila Pozze, Tasnia ya Kenya Imekufa! Somo limepatikana! Kwa Wote Mlioendelea Kunitumia Meseji Kuuliza Muziki Mpya, Say No more!,” alisema.

Willy Paul ambaye kwa sasa anafanya nyimbo za mapenzi baada ya kugura tasnia ya muziki wa Injili takriban miaka saba iliyopita alitoa wimbo wake wa mwisho ‘Kanyagaa’ takriban miezi miwili iliyopita. Wimbo huo hata hivyo ulikuwa tu sauti bila video.

Wimbo wa mwisho ambao bosi huyo wa Saldido Records alitoa na kuambatanisha na video ni ‘POPO’ ambao alimshirikisha Miss P Aprili mwaka huu.

Kwa upande mwingine, Bahati ambaye anadhaniwa kuwa mpinzani wake mkuu, alitoa wimbo mpya 'Salome' mapema wiki hii na pia amekuwa akifanya video za burudani na mkewe Diana Marua ili kuwaweka bize mashabiki wao.

Wawili hao ambao waligura tasnia ya muziki wa injili kwa nyakati tofauti miaka kadhaa iliyopita wamedaiwa kuwa mahasidi kwa muda mrefu na katika siku za nyuma wameonyesha wazi uhusiano mbaya kati yao hadharani.

Kuna uwezekano mkubwa kauli ya Willy Paul kuhusu wasanii kuachia muziki wakati wa mapumziko yake na kutopata matokeo mazuri ilikuwa shambulio lisilo la moja kwa moja kwa mwenzake, Bahati.