Mike Sonko akutana na mwanamke aliyemchora kwenye paja, akataa kumpa pesa

Sonko alionyesha nia ya kumsaidia mwanamke huyo kupata duka la nguo, akisema kwamba hawezi kumpa pesa mkononi.

Muhtasari

•Bi Njoki alimueleza Sonko kuhusu tamaa yake ya kuwa na duka la nguo katika mji wa Murang’a akisema anahitaji takriban Sh200,000 ili kuanzisha biashara hiyo.

•Sonko alimshauri mama huyo wa watoto wawili dhidi ya kuharakisha mambo, kuwa na watoto wengi wakati akiwa bado hajaimarika.

Image: TWITTER// MIKE SONKO

Siku ya Jumanne, aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko alikutana na mwanadada wa Murang’a ambaye alichora tattoo ya uso wake kwenye paja lake.

Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X, mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi alifichua kwamba alimkuta na Bi Mary Njoki akiwa amemsubiri ofisini mwake.

Sonko aliambatanisha taarifa yake na video ya mkutano wao mfupi ambapo walijadili mambo mbalimbali yakiwemo matatizo ya mwanadada huyo, maombi yake, sifa zake za masomo, familia yake, mipango ya baadaye, n.k.

"Nilisoma mpaka darasa la nane, sikuendelea siku na mtu wa kunisomesha," Bi Njoki alimwambia gavana huyo wa zamani.

Mama huyo wa watoto wawili aliendelea kumueleza Sonko kuhusu tamaa yake ya kuwa na duka la nguo katika mji wa Murang’a akisema anahitaji takriban Sh200,000 ili kuanzisha biashara hiyo.

Mfanyibiashara huyo tajiri alionyesha nia yake ya kumsaidia mwanamke huyo kupata duka na kuuza nguo, akisema kwamba hawezi kumpa pesa mkononi.

“Kwanza pata hiyo duka, alafu tutume watu wetu waione. Nitaongea na gavana wa huko ni rafiki yangu, ama Sabina Chege wote ni marafiki zangu,” Sonko alimwambia.

Aliendelea, “Waone duka, tulipie kama miezi sita ya kwanza. Stock lazima tuone ni wapi unanunua, tulipie. Hakuna pesa hapa, hakuna cash unapewa uende nayo. Kusema kweli huwa hatufanyi kazi hivyo, kama unataka pesa hiyo sahau. Hatupeani pesa.”

Gavana huyo wa zamani pia alichukua fursa hiyo kumshauri mama huyo wa watoto wawili dhidi ya kuharakisha mambo, kuwa na watoto wengi wakati akiwa bado hajaimarika.

Kwa upande mwingine, mwanasiasa huyo pia alimpa mwanamke huyo kazi ya muda katika ofisi yake huku wakisubiri kujua ni suluhisho gani bora kwake.

Bi Njoki alipoulizwa iwapo ataifuta tattoo ya Sonko kuona kwamba tayari amekutana naye na wakazungumza, mama huyo wa watoto wawili alisema, “Siwezi kufuta, haiwezi kutoka."

Hivi majuzi, Bi Mary Njoki alitengeneza video akiyoonyesha tattoo ya uso wa Sonko ambayo alichora kwenye sehemu ya juu ya paja lake la kushoto.

Katika video hiyo iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, alimwomba gavana huyo wa zamani amsaidie akitaja kwamba hayuko katika hali nzuri ya kifedha.

“Hi Sonko, Mike Sonko, Habari yako. Mimi ni Mary Njoki kutoka Murang’a. Mimi ndiye nilikuchora tattoo, na ndiyo hii hapa kwa mguu. Mimi napitia mashida nyingi sana, naomba tu unisaidie. Niko na watoto wanafaa ukubwa. Sina familia, sina wazazi. Ni watoto tu, niko pekee yangu mimi, na naomba tu unipee. Ata kama ni kazi, naomba tu unipe.

Watoto wangu wanataka kukula, kutaka kukunywa na kuomba tu ata kama ni kazi tu utanipea nitafanya, nitashukuru tu Mungu,” Bi Njoki alisema.

Akizungumzia sababu ya kuchora tattoo hiyo, mwanamke huyo alisema kwamba ukarimu wa Sonko ulimvutia na alitaka tu kumshangaza.

“Nakuomba tu Mike Sonko, nisaidie tu. Mungu atakubariki. Ndiye huyu mimi, na ndiyo hii tattoo hapa, mwanadada kutoka Murang’a,” alisema.