"Moyo wangu umezama kabisa!" Betty Kyallo azidiwa na hisia baada ya kufiwa na mpendwa

Betty alichukua muda kuwashauri watu kuwaweka karibu wapendwa wao hata wakiwa hai.

Muhtasari

•Betty alionekana akiwa amevunjika moyo sana na alibainisha kwamba  ilikuwa siku ya huzuni kwake baada ya kumpoteza mpendwa wake.

•Betty alipongeza kipaji cha marehemu  na kusema kuwa ulimwengu umempoteza msanii mbunifu na mtu mzuri kwa ujumla.

azidiwa na hisia akimuomboleza rafikiye
Betty Kyallo azidiwa na hisia akimuomboleza rafikiye
Image: INSTAGRAM// BETTY KYALLO

Siku ya Alhamisi, mwanahabari  na mfanyabiashara maarufu wa Kenya Betty Mutei Kyallo alikuwa na wakati wa hisia alipokuwa akimuomboleza rafiki  yake wa karibu ambaye alimtambulisha kama Migz.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Betty alichapisha video iliyomuonyesha akiwa ndani ya gari lake akionekana kuvunjika moyo sana na kubainisha kwamba  ilikuwa siku ya huzuni sana kwake baada ya kumpoteza mpendwa wake.

Pia alitumia fursa hiyo kuwashauri watu kuwaweka karibu wapendwa wao hata wakiwa hai.

"Nina huzuni sana leo. Waweke uwapendao karibu sana,” Betty alisema chini ya video hiyo aliyoiweka.

Mtangazaji huyo wa zamani aliendelea kuelezea uhusiano wake na marehemu akibainisha kuwa alikuwa mwanafunzi mwenzake katika Chuo Kikuu cha Daystar.

“Jamani, nawaambia nimekuwa na siku ya huzuni zaidi leo. Rafiki yangu, tulikuwa pamoja chuoni pale Daystar. Tulikuwa kama marafiki wazuri sana, tulikuwa marafiki sana, tulikuwa tumeelewana sana. Hili limekuwa jambo la kusikitisha tu!” Alisema Betty huku huzuni nyingi ikiwa imeandikwa usoni mwake.

Aliongeza, “Moyo wangu umezama tu. Moyo wangu umezama sana. Ujumbe ulikuwa mtu yeyote unayempenda, unapaswa kuwashikilia sana kwa sababu hujui."

Mama huyo wa binti mmoja pia alishiriki video za baadhi ya kazi za uchoraji zilizofanywa na marehemu, akifichua kwamba alikuwa msanii mzuri.

Aidha, alipongeza ustadi wa marehemu  na kusema kuwa ulimwengu umempoteza msanii mbunifu na mtu mzuri kwa ujumla.

"Ni hasara iliyoje ya mtu mwenye akili nzuri ya ubunifu na utu mzuri. Pumzika vizuri rafiki yangu Migz. Hakika ulikuwa malaika duniani,” alisema.

Betty hata hivyo hakushiriki maelezo zaidi kuhusu marehemu au nini kilisababisha kifo chake cha bahati mbaya.