Mwanahabari Makena Njeri abadilisha jina lake kuwa Chris Muriithi

Makena abadilisha maelezo yake ya jina kwenye Instagram kuwa Chris Muriithi.

Muhtasari

•Kwa muda mrefu sasa amekuwa wazi kuhusu jinsia yake na msimamo wake kuhusu masuala ya wapenzi wa jinsia moja.

•Makena/Muriithi alisimulia hadithi yake mwaka jana ambapo alifunguka kuhusu msimamo wake wa kijinsia.

Image: INSTAGRAM// MAKENA NJERI

Mtangazaji wa zamani wa BBC Makena Njeri amechukua hatua ya kubadilisha maelezo yake ya jina kwenye Instagram kutoka Makena Njeri kuwa Chris Muriithi.

Licha ya jinsi hatua hiyo inaweza kuonekana kuwa ya kutatanisha, kwa kweli sio ya kushangaza miongoni mwa wafuasi wake kwani kwa muda mrefu sasa amekuwa wazi kuhusu jinsia yake na msimamo wake kuhusu masuala ya wapenzi wa jinsia moja.

Makena ni mwanzilishi wa Bold Network Africa ambayo ni harakati ya utetezi na haki za jumuiya ya wapenzi wa jinsia moja, wenye jinsia mbili, waliobadili jinsia (LGBTQ). Hatua hii huenda ni kuunga mkono msimamo wake kwenye harakati hiyo.

Kwa sasa maelezo ya mwanahabari huyo kwenye Instagram yanasoma, "Chris Muriithi (wao), mtu mashuhuri, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Bold Network Africa. Vuguvugu shupavu la utetezi na haki kwa LGBTQ. Spika wa TedX, Mteule wa Emmy (Mwandishi wa habari), ninasonga tofauti,"

Makena/Muriithi alisimulia hadithi yake mwaka jana ambapo alifunguka kuhusu msimamo wake wa kijinsia.

Katika video iliyochapishwa na TedX, alisema ilimchukua miaka mingi kukubali na kukiri ukweli kwake mwenyewe.

Akizungumza zaidi kujihusu,  alikiri kuwa alipata afueni na furaha kubwa baada ya kupata ujasiri wa kuzungumzia jinsia yake.

"Naitwa Chris Njeri Makena, nina furaha, niko huru na nina ujasiri. Kwa muda mrefu sana, sikuweza kujitambulisha hivi lakini mahali fulani katika safari nilianza kugundua maana ya kuishi ukweli wako. Nilianza kugundua mimi ni nani na niliamua kuwa mwaminifu kwa uhalisi wangu." alisema.

Muigizaji huyo wa zamani wa 'Tahidi High' alisema kwa muongo mmoja uliopita, alijitahidi kuishi maisha ya kawaida, "kulingana na kanuni tofauti za kijamii ambazo zimewekwa juu yetu tangu umri mdogo sana".

"Nikiwa na umri wa miaka 19, nilipokuja mjini, nilitaka kuigiza na kuwa supastaa nikishiriki katika vipindi tofauti vya televisheni. Lakini nilijua kwa hakika kwamba vita nilivyokuwa nikipitia nikiwa kijana vitajaribiwa katika jiji hili, niligundua kuwa kile ambacho jamii ilitaka nichukue haikuwa hivyo kwa ubinadamu na mimi," alisema.

"Nakumbuka kwa mara ya kwanza katika maisha yangu baada ya miaka mingi sana nikijitazama kwenye kioo na nikajisemea, mimi ni shoga, mimi ni wa kipekee na huu ndio ukweli wangu."

Aliongeza kuwa baada ya hapo uzito uliinuliwa kutoka kifuani mwake kwani hatimaye alikuwa huru. "Huu ulikuwa ushindi kwangu bila kujua itakuwa safari ya ujasiri."