"Nilikutazama nikaona kila kitu nilichotaka kwa mwanamke," Guardian Angel akumbuka kukutana na Musila

Musila alisema wimbo wa mwimbaji huyo wa injili, 'Rada' ulikuwa mwanzo wa muungano wao wa kudumu.

Muhtasari

•Guardian Angel na Esther Musila waliadhimisha miaka mitatu tangu walipokutana kwa mara ya kwanza.

•Guardian Angel kwa upande aliweka wazi kuwa alimpenda mwanamke huyo wa miaka 53 baada ya kukutana naye.

Guardian Angel na mke wake Esther Musila
Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Siku ya Jumatatu, Machi 13, wanandoa maarufu Guardian Angel na Esther Musila waliadhimisha miaka mitatu tangu walipokutana kwa mara ya kwanza.

Esther Musila alisema wimbo wa mwimbaji huyo wa injili, 'Rada' ulikuwa mwanzo wa muungano wao wa kudumu. Alipata hamu ya kukutana na Guardian Angel baada ya kuusikia wimbo huo kwenye redio na kuupenda.

"Muungano wetu usingetokea kwa namna nyingine. Tulikuwa na mipango yetu lakini Mungu alitangulia mbele yetu na ameendelea kutuongoza katika safari yetu," alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa watoto watatu wakubwa alidokeza kwamba baada ya kukutana Guardian Angel kwa mara ya kwanza hakufikiria kwamba wangekuwa marafiki wakubwa na hatimaye kuwa mume na mke.

"Ninashukuru kuwa na wewe katika maisha yangu. Heri ya siku ya ukumbusho wa urafiki mume wangu @guardanangelglobal Nakupenda. ❤❤❤," aliandika.

Guardian Angel kwa upande aliweka wazi kuwa alimpenda mwanamke huyo wa miaka 53 baada ya kukutana naye. Katika taarifa yake, Angel alisema alipomwangalia Bi Musila aliona sifa zote anazohitaji kwa mke ndani yake.

"13/3/2020 ulinitazama ukaona supastaa. Hamu yako ilikuwa kuniona nikiwa vile ulivyoniona. Nilikutazama na kuona kila nilichotaka kwa mwanamke. Miaka mitatu baadaye sisi sote tuna kile tulichotaka," alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 alimtaja Bi Musila kuwa mke mzuri na kukiri mapenzi makubwa kwake. 

"Sikukosea na ninafurahi kwamba Mungu ametimiza kweli na ataendeleza kusudi langu katika maisha yako. Asante kwa Kuja. Nakupenda ❤❤," Musila alijibu.

Hivi majuzi,Musila alifichua kuwa kuna wanaume wengi ambao wamekuwa wakimtongoza kwa jumbe tamu za mapenzi licha ya yeye kuwa kwenye ndoa tayari.

Akizungumza na waandishi wa habari, mama huyo wa watoto watatu wakubwa alieleza kuwa kurasa zake za mitandao ya kijamii zimejaa jumbe tamu za mahaba kutoka kwa wanaume ambao wamekuwa wakimmezea mate.

Musila hata hivyo aliweka wazi kwamba huwa anapuuza jumbe hizo na hata kufuta baadhi yake ambazo zimepita mipaka.

"Huwa zinakuja (Jumbe) lakini huwa nazipuuza tu. Zile ambazo zimekithiri huwa nafuta na kublock," alisema.

Alisema kuna wanaume wengi ambao wako tayari sana kuangusha ndoa yake ya zaidi ya mwaka mmoja na Guardian Angel.

"Ni wengi sana. Lakini hakuna nafasi ya kuwatumbuiza," alisema.