Orodha ya mastaa wa Kenya na Tanzania ambao wamewahi kuchumbiana/kufunga ndoa

Diamond na Tanasha walichumbiana kwa kipindi kifupi kati ya 2019-2020.

Muhtasari

•Ben Pol alijitosa kwenye mahusiano na Anerlisa mwaka wa 2018 kabla ya kufunga pingu za maisha naye mwezi Mei 2020.

•Ali Kiba na Amina Khalef walifunga ndoa mwaka wa 2018 na wakabarikiwa na watoto wawili pamoja kabla ya kutalikiana mwaka jana.

Ben Pol na Anerlisa Muigai
Image: HISANI

Katika kipindi cha siku chache zilizopita, wanandoa wa zamani Ben Pol na Anerlisa Muigai wamekuwa mada katika majukwaa mengi ya udaku na habari.

Wawili hao walianza kuvuma mwishoni mwa wiki jana kufuatia mahojiano ya Ben na Millard Ayo ambapo mwimbaji huyo alikiri kuwa hakuwahi kufurahia ndoa yao.

Ben Pol ambaye ni Mtanzania alijitosa kwenye mahusiano na binti huyo wa seneta wa Nakuru, Kenya Tabitha Karanja mwaka wa 2018 kabla ya kufunga pingu za maisha naye mwezi Mei 2020. Wawili hao walitengana mwezi Februari mwaka  wa 2021.

Ben Pol na Anerlisa sio watu mashuhuri wa kwanza kutoka Kenya na Tanzania kuwahi kuzama pamoja kwenye dimbwi la mahaba. Chini hapa kuna wasanii na watu wengine mashuhuri kutoka Kenya na Tanzania ambao wamewahi kuchumbiana.

  •  Diamond Platnumz na Tanasha Donna

Bosi huyo wa WCB aliwahi kuwa kwenye mahusiano na mwanamuziki Tanasha Donna kutoka Kenya. Wawili hao walichumbiana kwa kipindi kifupi kati ya 2019-2020.

Katika kipindi cha mahusiano yao, wasanii hao walijaliwa mtoto mmoja pamoja anayejulikana kama Naseeb Junior.

  •  Alikiba na Amina Khalef

Staa wa Bongo Ali Saleh Kiba almaarufu Alikiba alikuwa kwa ndoa na mrembo kutoka Mombasa, Amina Khalef.

Wawili hao walifunga ndoa mwaka wa 2018 na wakabarikiwa na watoto wawili pamoja kabla ya kutalikiana mwaka jana.

Ndoa yao ilitamatika rasmi mwaka jana baada ya Bi Amina kuwasilisha talaka katika mahakama ya kadhi mapema mwaka huo. 

  • CMB Prezzo na Amber Lulu

Mwanamuziki mkongwe wa Kenya Jackson Makini almaarufu CMB Prezzo alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanasoshalaiti mashuhuri wa Tanzania Amber Lulu kati ya mwaka wa 2017 na 2018.

  • AY na Amani

Staa wa Bongo Ambwene Allen Yessayah almaarufu AY na malkia wa muziki wa Kenya Amani walikuwa kwa ndoa kwa takriban miaka miwili.

Wasanii hao wawili walifunga pingu za maisha mwaka wa 2005 ila ndoa yao ikagonga ukuta mwaka wa 2007.

  • Vera Sidika na Dkt Jimmy Chansa

Daktari mashuhuri wa Tanzania Jimmy Chansa alimchumbia mwanasoshalaiti wa Kenya Vera Sidika kwa kipindi kifupi mwaka wa 2019.

  • Jux na Huddah Monroe

Mwaka jana, staa wa Bongo R&B Juma Jux alidaiwa kuwa kwenye mahusiano na mwanasoshalaiti wa Kenya Huddah Monroe.

Wawili hao walionekana wakikumbatiana na kupigana busu hadharani mara kadhaa kati ya mwezi Juni na Julai.

Hata hivyo walijitokeza na kutupilia mbali madai ya mahusiano huku wakieleza kuwa uhusiano wao ni wa kirafiki tu.