Paula akabiliana vikali na mama yake Kajala baada ya Rayvanny kumtembelea kisiri

Paula alikuwa amemleta Rayvanny katika kikao kilichokusudiwa kwa familia tu, jambo ambalo liliamsha hasira za Kajala.

Muhtasari

•Wawili hao walikabiliana kwa maneno baada ya Paula kumwalika Rayvanny kwenye kikao cha kambi ambacho kilikusudiwa kuwa cha familia tu.

•Paula alimjibu mamake kwa kumkumbusha kuwa pia yeye ana maisha yake na kuwa hakuwahi kumhoji alipokwenda kwa Harmonize.

Paula, Kajala, Rayvanny
Image: INSTAGRAM

Filamu ya maisha halisia  ‘Behind The Gram’ inayomhusisha muigizaji Kajala Masanja na bintiye Paula Paul inaendelea kwenye Zamaradi TV.

Katika kipindi cha hivi punde, kutoka siku za nyuma, wawili hao walikabiliana kwa maneno baada ya Paula kumwalika aliyekuwa mpenzi wake wa wakati huo, Rayvanny kwenye kikao cha kambi ambacho kilikusudiwa kuwa cha familia tu.

Kajala alionekana akikimbia kwenye hema la Paula huku akiwa amefura kwa hasira kabla ya kumuuliza alikuwa na nani mle ndani.

"Paula, Paula. Hebu niambie nini kimefanyika? Nani huyo nimeona akitoka hapa sasa hivi? Niko serious. Nani amekuwa hapa," Kajala Masanja alisikika kujawa na ghadhabu alisikika akimuuliza binti yake Paula.

Katika majibu yake, mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 kwa ujasiri alimwambia mama yake kwamba ni mwanamuziki Rayvanny ambaye alikuwa naye kwenye hema yake. 

Kajala aliyejawa na hasira alimkumbusha kuhusu mipango ya kikao hicho na kumuuliza kwa nini alichukua hatua ya kumwalika bosi huyo wa NLM.

"Dada (dadake aliyeandamana naye) tumekuja huku kufanya nini, na tulitakiwaa kuja wangapi labda, na kwa nini umlete Ray wakati unajua mimi nipo. Kwa hivyo hujali kunihusu," Kajala alimfokea bintiye.

Paula alimjibu mamake kwa kumkumbusha kuwa pia yeye ana maisha yake na kuwa hakuwahi kumhoji alipokwenda kwa Harmonize.

"Mimi nilikuacha ukaenda kwa Harmo, nikakaa mwenyewe. Na mimi niko na maisha yangu. Wewe ulijali," Paula alijibu.

Kajala alionekana kutopendezwa na majibu ya bintiye na alikuwa tayari kumpiga kabla ya dada yake aliyekuwa nao kuwazuia wasipigane. Aliwaambia hakuna haja ya kupigana na kumuomba Paula amheshimu mama yake.

Wiki chache zilizopita, muigizaji Kajala Masanja aliweka wazi kwamba hakufurahi wakati alipogundua kwamba binti yake Paula yupo kwenye mahusiano na Rayvanny, takriban miaka miwili iliyopita.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha humu nchini, Kajala alisema pia yeye alikuja kufahamu kuhusu mahusiano hayo kupitia mitandao ya kijamii kama wanamitandao wengine wote.

"Paula hata hakuwa na nguvu za kuniambia. Ilitokea tukaona huko mitandaoni. Alikuwa 18. Kwa mawazo yangu nilijua Paula hana mpenzi," alisema.

Kajala alikiri kwamba alijaribu sana kumshauri mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 dhidi ya mahusiano na bosi huyo wa Next Level Music lakini juhudi zake  ziliangukia patupu kwani Paula hakusikia.

"Nilijaribu sana kumweleza kwamba hii sio sahihi lakini mtu anaenda anafanya kinyume, inabidi umeacha tu. Ukimwambia asiende na huyo mtu anasema sawa lakini bado anaendelea. Nilijaribu kumzuia sana," alisema.

Aidha, alisema baada ya kushindwa kumshauri Paula dhidi ya uhusiano huo, alimshauri jinsi ya kujiendeleza katika mahusiano.

"Nilimwambia kwa sababu yeye bado ni mdogo atulie bado ana maisha mbele. Asifanye vitu kwa hasira," alisema.

Kajala alisema alifurahi wakati mahusiano ya bintiye na Rayvanny yaligonga mwamba kwa sababu hakuona ndoa pale.