"Usishikilie ya zamani, acha yaende" Karen Nyamu ashauri wiki chache baada ya kumtema Samidoh

Nyamu aliwashauri Wakenya kuendelea kuwa wazi na wastahimilivu.

Muhtasari

•Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa watoto watatu aliwashauri Wakenya dhidi ya kushilia yaliyopita.

•Haya yanajiri wiki chache tu baada ya yeye kukatiza uhusiano na mpenzi wake wa muda mrefu, Samidoh.

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Wakili na seneta wa kuteuliwa aliyezingirwa na utata mwingi Karen Nyamu amewashauri watu kujifunza kuacha ya zamani.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa watoto watatu aliwashauri Wakenya dhidi ya kushilia yaliyopita.

"Usishikilie ya zamani, acha yote yaende kwa uzuri. Kila kitu kinakaribia kubadilika na kuwa bora," alisema siku ya Jumamosi.

Mwanasiasa huyo aliendelea kuwasihi watu kutopoteza matumaini na badala yake kuendelea kuwa wazi na wastahimilivu.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya yeye kukatiza uhusiano na mpenzi wake wa muda mrefu Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Karen alitangaza mwisho wa uhusiano wake na baba huyo wa watoto wake wawili katikati mwa Desemba kufuatia tukio la ugomvi uliowahusisha wao na mke wa Samidoh Edday Nderitu katika eneo moja la burudani jijini Dubai.

"Wanawake wakubwa na wajasiri watathibitisha kwamba mara nyingi kiungo chetu dhaifu ni wanaume tunaojihusisha nao. Ninaacha mtindo huo," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram mwezi jana.

Aliongeza "Nimefanya uamuzi wa kusitisha uhusiano wangu na baba wa watoto wangu na sasa ni mpenzi wa zamani."

Nyamu alibainisha kuwa hakuwa na majuto yoyote kufuatia  kile kilichotokea Dubai, na kuahidi kuwa tukio hilo lilikuwa la mwisho.

"Sitamani ningefanya mambo kwa njia tofauti," Nyamu alisema. "Najua nilipaswa kumpigia simu na kumaliza kimya kimya, lakini niliamua kuweka hadharani kama jinsi tu drama mambo tatanishi yamekuwa," aliongeza.

Hapo awali, Karen Nyamu, Samidoh na Edday Nderitu walikuwa wamehusika katika ugomvi ambao ulirekodiwa na video kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Wakenya watumizi wa mitandao ya kijamii walizungumza kuhusu drama hiyo kwa siku kadhaa huku wakitoa maoni tofauti kuhusu yaliyotokea.

Baadhi ya wanachama wa  UDA pia walikuwa wameomba kutenguliwa kwa uteuzi wa Nyamu kufuatia drama alizohusika.