Yahuzunisha! Mvulana mdogo aongoza waombolezaji kumzika rafikiye aliyeporomokewa na nyumba (+video)

Marehemu Joseph ,4, alipoteza maisha baada ya tingatinga kugonga kuta za nyumba aliyokuwamo na kumwangukia.

Muhtasari

•Eric alisaidia familia moja kumzika mtoto wao aliyefariki wakati wa ubomoaji wa nyumba wa hivi majuzi katika mtaa wa Mukuru Kwa Ruben, Nairobi.

•Eric alitumia fursa hiyo kuitaka serikali kumsaidia mwanamke huyo kwa madai kuwa mwanawe aliuawa na lori za serikali.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji Eric Omondi, kupitia vuguvugu lake la Team Sisi kwa Sisi alisaidia familia moja kumzika mtoto wao mchanga aliyefariki wakati wa ubomoaji wa nyumba wa hivi majuzi katika mtaa wa Mukuru Kwa Ruben, Nairobi.

Mtumbuizaji huyo, ambaye amegeuka kuwa mwanaharakati alikuwa amewahamasisha Wakenya kuchangia mazishi ya mvulana huyo wa miaka minne na pia kumsaidia mamake aliyeachwa na maumivu ya moyo.

Siku ya Jumatano, Eric alichapisha video yenye hisia  mazishi hayo yaliyofanyika katika makaburi ya Lang’ata. Video hiyo ilionyesha mvulana mdogo akiwaongoza waombolezaji kuelekea eneo la maziko huku Eric akifuata nyuma huku akisaidia kubeba jeneza.

“Mvulana anayetembea mbele ya Jeneza ni Emmanuel, Alikuwa Rafiki mkubwa wa Joseph (Marehemu). Walikuwa pamoja wakati wa ubomoaji Bulldozer ilipoangusha kuta na kumwangukia rafiki yake, alikuwa na bahati,” Eric Omondi alisema chini ya video hiyo.

Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show aliendelea kufichua jinsi alivyotumia pesa zilizochangishwa na Wakenya kumsaidia mama huyo ambaye alisema alikuwa na uchungu mwingi.

 “Tumemlaza Joseph leo Langata. Mama yake hayuko sawa hata kidogo. Tumemlipa Kodi ya Mwaka Mmoja, pia tumemnunulia vitu vya nyumbani na tumemfungia 150,000 kwenye akaunti ili amfungulie biashara atakapokuwa tayari,” alisema.

Pia alitumia fursa hiyo kuitaka serikali kumsaidia mwanamke huyo kwa madai kuwa mwanawe aliuawa na lori za serikali.

“TUNATOA WITO KWA SERIKALI KUMFIDIA MWANAMKE HUYU Kwa Sababu Mwanae ALIUWAWA na Mabuldoza ya Serikali. ASANTE TEAM SISI KWA SISI. MUNGU AWABARIKI,” alisema

.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya mchekeshaji huyo, marehemu Joseph alipoteza maisha baada ya tingatinga kugonga kuta za nyumba aliyokuwamo na kumwangukia.

Pia aliripoti kuwa kufuatia tukio hilo la kusikitisha, mama wa mvulana huyo alijaribu kujitoa uhai kwa sababu ya uchungu lakini majirani walimzuia.