Gavana Mike Sonko aachiliwa kwa dhamana ya milioni 15

mike.sonko
mike.sonko
Gavana wa Nairobi Mike Sonko amepewa dhamana ya milioni 15 au bondi ya milioni 30.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Kupambana na Ufisadi Douglas Ogoti katika uamuzi wake Jumatano pia alizuia Sonko kufika ofisini mwake akisema bosi wa kaunti ya Nairobi anaweza kusindikizwa kuchukua vifaa vyake kutoka City hall.

Ogoti alisema amezingatia mashtaka yote, hasara zilizotokea, aina ya makosa na kiasi kinachohusika katika kila mtu anayeshtakiwa.
Hakimu pia alimwambia Sonko ahakikishe wafuasi wake hawasababishi machafuko na akamwonya asiwashawishi wafanye vivyo.
Washtakiwa wote pia walizuiliwa kukaribia au kuwasiliana na mashahidi katika kesi hii.
Katika kujaribu kupinga ushahidi, Sonko alikuwa ametoa hati ya mwenendo mzuri mahakamani na tuzo za balozi wa matendo mema.

Katika uamuzi wake, Ogoti alizuia mshtakiwa kutoa maoni ya kesi hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Gavana huyo ameshtakiwa kwa utapeli wa pesa na uporaji haramu wa mali ya umma kiasi cha milioni 357 milioni, City hall.
Anashutumiwa pia kukabidhi zabuni kwa wasaidizi wake wa karibu, kughushi nyaraka na matumizi mabaya ya fedha za kaunti.
Mike Sonko hata hivyo alikana mashtaka yote siku ya Jumatatu.

Ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ilipinga kuachiliwa kwa Sonko kwa dhamana.