Wakenya kunusuriwa na mipango ya wizara ya uchukuzi kutibidhi nauli

Kwa muda, wakenya wamekua wakinyanyaswa mikononi mwa wamiliki wa magari ya uchukuzi wa umma.

La kustaajabisha ni kuwa kwa miaka mingi, serikali kuu imekosa kuingilia kati na kutatua hali ya kupandisha nauli barabarani.

Wenyeji wa mji Nairobi ndio ambao wamekumbwa na changamoto hii, ambapo nauli huongezwa nyakati za asubuhi, jioni au katika msimu wa mvua.

Katika mwezi wa kumi na moja mwaka jana, serikali iliweza kurejesha sheria za barabara, almaarufu Michuki Rules kwa minajili ya kupunguza ajali amabazo zilikua zimekitiri barabarani.

Katika hali hiyo, baadhi ya magari ya uchukuzi yalishindwa kutekeleza kanuni hizo na kujiondoa barabarani, jambo lililosababisha magari kua chache na kuongeza nauli.

Mapema mwaka huu, wenyeji wa kaunti ya Bomet waliandamana na kuwalaumu wamiliki wa magari ya uchukuzi wa umma kwa kuongeza nauli mara dufu, jambo lililowakera mno.

Wenyeji hao walitoa wito kwa waziri wa usalama wa ndani ya nchi Fred Matiang’i kuingilia kati na kutatua changamoto hiyo.

Hapo jana, katibu mkuu katika wizara ya uchukuzi Chris Obure alifika katika kamati ya bunge inayohusika na maswala ya uuma na nyumba na kupendekeza mabadiliko kadhaa katika sekta ya uchukuzi.

Mbele ya kamati inayoongozwa na mbunge David Pkosing, Obure alisema wizara hiyo inapendelea kurekebisha ibara ya 119(1) ili kuwezesha wizara ya uchukuzi kutibidhi na kutoa mwelekeo wa nauli inayotozwa na magari ya uchukuzi wa umma.

Matamshi ya Obure yalipokelewa na wakenya na kuonekana kufurahishwa na mikakati hiyo. Baadhi yao wamesema wamekua wakilipia nauli ya juu licha ya bei ya petrol na diseli kupunguzwa.