Kaza mkanda, hali ngumu kiuchumi yaja, bajeti ya kitaifa yapunguzwa

Kamati ya Bunge ya bajeti imeidhinisha makadirio ya matumizi ya pesa za serikali kipindi  cha mwaka 2019-2020 baada ya kuafikiana na wizara ya fedha katika mazungumzo yaliofanyika siku ya Jumanne.

Hatua hii itampa ruhusa waziri Rotich kusoma bungeni bajeti ya kitaifa kwa kipindi kijacho cha matumizi ya pesa za serikali Alhamisi wiki ijayo.

Katika ripoti hiyo kamati ya bajeti ilisema walilazimika kuifanyia ukarabati bajeti hiyo kutokana na changamoto za matarajio ya ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kulingana na makadirio hayo, bajeti za Bunge, serikali na mahakama ni jumla ya shilingi trilioni 3.02.

Hii anamaanisha bajeti ya mwaka huu imepunzwa kwa takriban asilimia 4.2 ikilinganishwa na kipindi cha kifedha cha mwaka uliyopita.

Serikali ya kitaifa imetengewa shilingi trilioni 1.84, serikali za kaunti zitapokea shilingi bilioni 371.6, bunge litapokea bilioni 43 huku idara ya mahakama ikipokea shilingi bilioni 18.8.