Dereva na makanga wauaji wapokonywa leseni

Mamlaka ya kitaifa usalama barabarani NTSA imefutilia mbali leseni za kuhudumu za Dereva wa matatu Joseph Muasya na manamba John Ndwai kwa kosa la kumsukuma nje abiria wakati gari lilipokuwa linaenda.

Mhasiriwa Florence Wanjiru alifariki kutokana na majeraha aliyopata baada ya kusukumwa nje ya matatu inayomilikiwa na Killeton SACCO yenye nambari za usajili KCC 086U. Mkurugennzi mkuu wa NTSA Francis Maja alisema dereva huyo na manamba wanazuiliwa na polisi wakisubiri kufunguliwa mashtaka.

Meja alisema kwamba mamlaka hiyo imegiza maafisa wa Killeton SACCO kuwasilisha ripoti kamili kuhusu nini kilepelekeo Wanjiru kurushwa nje ya gari lililokuwa likienda. Wanjiru aliyekuwa na umri wa miaka 28 alikuwa mfanyikazi katika Yongli Casino mtaani Hurlingham Nairobi.

Uchunguzi wa polisi umebaini kuwa Wanjiru aliabiri matatu ya kwenda katikati mwa jiji la Nairobi mnamo Juni tareje tano mwaka huu katika kituo cha basi cha Kilimani. Ripoti za awali za polisi zilikuwa zimeonysha kwamba kilikuwa kisa cha kawaida cha kugongwa na gari na dereva kutoroka.

Mlinzi mmoja alimuona Wanjiru akiwa amelala barabarani akilia kwa uchungu na kutumia simu yake kuwapigia jamaa wake.

Mhasiriwa alikimbizwa katika hospitali ya St Francis ambapo madaktari walisema kwamba hali yake ilikuwa mbaya.

Alihamishiwa katika Hospitali ya kitaifa ya Kenyatta ilipogunduliwa kuwa ubongo wake ulikuwa umevuja na fuvu la kichwa chake kupasuka, alifariki siku tatu baadaye akipokea matibabu.