Sakaja azungumzia madai ya kuzozana na naibu rais Rigathi Gachagua

Sakaja alibainisha kuwa hana mzozo wowote na Gachagua, akiongeza kuwa Naibu Rais ni kiongozi mzuri anayehitaji heshima.

Muhtasari
  • Gavana huyo alitetea uhusiano wake na Gachagua, akisisitiza hajawahi kuzungumza vibaya kuhusu aliyekuwa mbunge wa Mathira.
Gavana Sakaja ndani ya studio za Radio Jambo
Image: BRIAN SIMIYU

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amekanusha madai ya kutoelewana kisiasa kati yake na Naibu  Rais Rigathi Gachagua.

Akihojiwa kwenye runinga ya NTV, Sakaja alisema kiongozi wa pili ni mkuu wake na kiongozi anayeheshimika katika jamii.

Sakaja alibainisha kuwa hana mzozo wowote na Gachagua, akiongeza kuwa Naibu Rais ni kiongozi mzuri anayehitaji heshima.

“Mimi sina mgogoro na naibu rais. Ni mkubwa wangu anaeheshimika na amekuwa kwenye siasa japo aliingia kwenye siasa baada yetu japo aliingia na kuwa maarufu. Ni kiongozi mzuri anayepaswa kuheshimika. ", Sakaja alisema.

Gavana huyo alitetea uhusiano wake na Gachagua, akisisitiza kuwa hajawahi kuzungumza vibaya kuhusu aliyekuwa mbunge wa Mathira.

"Sijawahi kumsema vibaya. Sijawahi kumtaja. Ninamheshimu kama kiongozi wetu, makamu wa rais, na naibu kiongozi wa chama," Sakaja alisema.

Gavana huyo pia alitangaza kwamba hatazamii nafasi yoyote katika Muungano wa Kidemokrasia (UDA).

"Sitaki kuwa Naibu wa Rais au Naibu Kiongozi wa Chama, kwa sasa nina Kaunti ya Nairobi ambayo ni mtazamo wangu isipokuwa Rais aseme anataka ujuzi wangu katika chama, kwa sasa mimi ni mtumishi wa watu" , alisema.