Tutajenga kilabu ya usiku katika bustani ya Uhuru Park - Sakaja

Sakaja alisema hii itawafungulia watu njia ya kufungua vilabu vya usiku katika uwanja huo.

Muhtasari

•"Kuna kilabu ya usiku ambayo itakuwa hapa. Tulikubaliana hiyo kupiga kelele kwa estate muache. Unaweza kuja hapa na kupiga kelele hadi ng'ombe warudi nyumbani," alisema.

•Gavana huyo alitoa wito kwa umma haswa wakazi wa Nairobi kulinda mbuga hiyo na kuepuka vitendo vyovyote vya uharibifu.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale akiwa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja wakati wa kukabidhi bustani ya Uhuru Park kwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi mnamo Aprili 18, 2024.
Waziri wa Ulinzi Aden Duale akiwa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja wakati wa kukabidhi bustani ya Uhuru Park kwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi mnamo Aprili 18, 2024.
Image: HISANI

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ametangaza ujenzi wa kilabu ya usiku katika bustani ya Uhuru Park.

Sakaja alisema hii itawapa watu njia mbadala ya kufunguliwa kwa vilabu vya usiku katika uwanja huo.

"Kuna kilabu ya usiku ambayo itakuwa hapa. Tulikubaliana hiyo kupiga kelele kwa estate muache. Unaweza kuja hapa na kupiga kelele hadi ng'ombe warudi nyumbani," alisema.

"Hiyo ndiyo sehemu, sherehe mfanyie hapo."

Alisema miradi ya ziada katika bustani hiyo ambayo pia inajumuisha migahawa ya Waswahili na ya Kiafrika miongoni mwa mingine itajengwa chini ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPPs).

Maeneo mahsusi yatakapowekwa vifaa hivyo, alisema, tayari yametambuliwa na kuwahakikishia wale wanaopenda kuendesha biashara hizo miongoni mwa wengine katika hifadhi hiyo kuwa mchakato huo utakuwa wa uwazi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hifadhi hiyo iliyotengenezwa na Wizara ya Ulinzi, Sakaja alisema hivi karibuni watafungua mchakato wa utoaji zabuni kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma na Uondoaji wa Mali (PPDA).

Wakati uo huo, gavana huyo alitoa wito kwa umma haswa wakazi wa Nairobi kulinda mbuga hiyo na kuepuka vitendo vyovyote vya uharibifu.

Aliwaambia wazingatie sheria za hifadhi ambazo ziko kwenye lango la kituo hicho.

Alibainisha kuwa shughuli zinazofanywa zilikuwa na gharama kubwa.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale akiwa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, maafisa wengine na maafisa wa usalama wakati wa kukabidhi bustani ya Uhuru Park kwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi mnamo Aprili 18, 2024.

“Tujitolee katika kuitunza na kuiboresha hifadhi hii na mbuga nyinginezo kote jijini,” alisema huku akiwataka waliovamia kuhama mara moja.

"Kila aliyevamia hifadhi fanya mwenyewe tu ili tukija usiseme tumebomoa maana hatutoki mpaka tuirejeshe."

City Park, aliongeza, inatazamiwa kukabidhiwa kaunti kutoka kwa Huduma ya Misitu ya Kenya (KFS).

Mnamo Novemba 2022, Jumba la Jiji lilighairi leseni za vilabu vya usiku ambavyo vilikuwa vikifanya kazi katika maeneo ya makazi na kusema kuwa haitakuwa ikitoa vibali vya majengo kama hayo tena.

Sakaja alisema kuendelea mbele, leseni za vilabu vya usiku zitatolewa tu kwa majengo yanayofanya kazi ndani ya Wilaya ya Biashara ya Kati na mitaa iliyoainishwa ndani ya maeneo maalum ya makazi.