Uhuru kujitenga na kampeni za Kibra

Rais Uhuru Kenyatta hatamfanyia kampeni mgombeaji wa Jubilee Macdonald Mariga katika uchaguzi mdogo wa Kibra.

Wandani wa rais walisema “ ana mambo muhimu sana ya kitaifa kushughulikia na hakuwa na mipango ya kufanya kampeni Kibra”.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena hakujibu maombi yetu kuzungumzia swala hili kufikia Jumatatu saa moja jioni. Tume ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) ilimuidhinisha Mariga siku ya Jumatatu kuania kiti cha ubunge cha Kibra na kufungua uwanja wa kuonyeshana ubabe wa kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga.

Mariga anatarajia kupata uungwaji mkono kutoka kwa Naibu rais William Ruto pamoja na viongozi wengine wa Jubilee, wakiwemo kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen na mbunge wa Lang’ata Nixon Korir – ambao ni wandani sana wa Ruto.

Katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju ndiye afisa wa juu zaidi wa Jubilee kutoka mrenkgo wa rais Kenyatta aliyekuwepo wakati wa hafla ya kupeana cheti cha uteuzi kwa Mariga. Inaaminika kwamba Uhuru hataki kushiriki kampeni za Kibra kwa sababu huenda zikahujumu ushirikiano wake na Raila Odinga.

Raila alikuwa mbunge wa Lang’ata iliyojumuisha eneo la Kibra kwa kipindi cha miaka15, na kwa muda sasa anauungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo. Eneo bunge hilo liligawanywa mara mbili Lang’ata na Kibra.

Uchaguzi huu mdogo wa Novemba 7 unaonekana kuwa malumbano ya ya kuavua misuli ya ubabe kati Raila na Ruto kutumiwa kupasha misuli kwa uchaguzi wa mwaka 2022. Imran Okoth kakake marehemu aliyekuwa mbunge wa eneo hiko Ken Okoth atapeperusha bendera ya ODM.