Margaret Kenyatta apongezwa kwa juhudi za kupambana na ukimwi

Mkurugenzi mpya wa shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na maradhi ya ukimwi Dkt. Medhin Tsehaiu amempongeza Mama wa Taifa Margaret Kenyatta kutokana na wajibu wake katika vita dhdi ya maradhi hayo hapa nchini.

Dkt. Tsehaiu ambaye aliteuliwa mwezi Julai mwaka huu alisema Mama wa Taifa Margaret Kenyatta, kupitia Shirika lake la Beyond Zero amechangia pakubwa katika kupunguza maambukizi ya maradhi ya ukimwi hususan kutoka kwa akina mama hadi watoto wachanga.

“Nakupongeza kwa uongozi wako na kujitolea katika juhudi zetu za kukabili maambukizi ya ukimwi kutoka kwa akina mama hadi watoto wachanga. Tunashukuru sana kwa usaidizi wako," Dkt. Tsehaiu kamwambia Mama wa Taifa alipomtembelea katika Ikulu ya Nairobi.

Dkt. Tsehaiu alimfahamisha Mama wa Taifa kutokana na mipango kabambe ya shirika lake kupunguza maambukizi ya maradhi hayo kwa kuhakikisha kwamba itimiapo mwaka 2020 asilimia 90 ya watu wanaoishi na maradhi ya ukimwi wataifahamu hali yao ya afya, kupewa dawa za kupunguza makali na kupunguza kabisa kuongezeka kwa virusi.

Mkurugenzi huyo wa shirika la Umoja wa Mataifa hapa nchini alisema Kenya inaendelea kupiga hatua katika vita dhidi ya maradhi hayo na akatoa wito wa njia bunifu  zinazowavutia vijana wengi ambao wanakumbwa na hatari kubwa.

"Nchi iko katika mwelekeo mzuri kwa sababu ya kujitolea na uongozi bora. Huku tukikaribia hatua za mwisho, sharti tufanye mambo kwa njia tofauti ambayo ni bunifu,” kasema Dkt. Tsehaiu.

 Mama wa Taifa Margaret Kenyatta alimhakikishia Mkurugezi huyo wa shirika la UNAIDS kujitolea kwake kikamilifu kukabili maradhi ya ukimwi.

“Kama ilivyo kawaida, mnaweza kunitegemea kuhusiana na mipango hii ya maana,” kasema Mama wa Taifa akiongeza kwamba ufanisi ulioafikiwa katika miaka ya hivi majuzi ikiwemo juhudi za kupungua kwa maambukizi miongoni mwa watu wazima kwa kiwango cha nusu kutoka visa 101,000 hadi 46,000 mwaka jana zapaswa kudumishwa.

Mapema, Mama wa Taifa Margaret Kenyatta alifanya mashauri na Mkurugenzi Mfawidhi wa Wakfu wa Mpango wa Kutetea Ndovu Miles Anthony Sloan Geldard.

Mpango wa Kulinda Ndovu ni shirika linalojumuisha mataifa 20 ya Afrika yaliyojitolea kuangamiza uwindaji wa ndovu.

Bw. Geldard ambaye alimpongeza Mama wa Taifa kwa juhudi zake katika uhifadhi wa ndovu hapa nchini pia alimwarifu kuhusu mkutano wa hivi majuzi wa Mkataba kuhusu Biashara ya Kimataifa katika Wanyama walio Hatari ya Kuangamia uliofanyika nchini Uswizi.

Mama wa Taifa alielezea kuridhika kwake na maendeleo ambayo yameafikiwa katika kupigwa marufuku kwa biashara ya pembe za ndovu note ulimwenguni na akamhakikishia Bw.  Geldard  ataendelea kuunga mkono ajenda ya uhifadhi.

Mama wa Taifa Margaret Kenyatta na mwenzake wa Sierra Leone Fatima Maada Bio waliteuliwa katika Baraza la Uongozi la Mpango wa Kulinda Ndovu linaloongozwa na aliyekuwa Rais wa Botswana Ian Khama.

-PSCU