HPV: Kenya yazindua chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, ina umuhimu gani?

hpv
hpv
Kenya imezindua kampeni ya kitaifa kuwachanja wasichana dhidi ya HPV, kirusi kinachohusishwa kusababisha baadhi ya saratani ikiwemo ya shingo ya uzazi.

Ni taifa la 16 barani Afrika kuidhinisha mpango huu wa chanjo dhidi ya HPV. Chanjo hiyo inatolewa kwa watoto wenye umri wa miaka 10 na maafisa wanatumai kuwafikia watoto laki nane katika mwaka wa kwanza wa uzinduzi.

Rais Uhuru Kenyatta ameizindua rasmi kampeni hiyo leo katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya huku akitoa wito kwa raia kushikilia usukani wa afya zao kwa kuhakikisha wanafanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara wa saratani.

Kwanini chanjo ya HPV ni muhimu?

Saratani ya shingo ya uzazi huwaathiri zaidi ya wanawake nusu milioni kila mwaka na husababisha vifo vya wanawake laki mbili na nusu kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO. Ni mojawapo ya saratani inayowashika wengi hii leo lakini pia ni mojawapo ya saratani inayoweza kuzuilika.

Chanjo dhidi ya HPV hulinda usalama dhidi ya maambukizi yanayohusishwa kwa karibu na saratani hiyo, na ukaguzi wa mapema husaidia kutambua seli kabla hazijageuka saratani. Uzinduzi wa chanjo hii sasa nchini kenya unakuja wakati ambapo shirika la madaktari wa Kanisa Katoliki nchini Kenya (KCDA), limekuwa likipinga mpango huo wa kutoa chanjo ya HPV kwa watoto wasichana wa miaka 10 kutokana na madai ya kuwepo kwa madhara yake ikiwemo kuharibika ubongo, kifafa au kupooza mwili.

Hatahivyo hakuna madhara yaliyoripotiwa katika mataifa ambayo yameidhinisha chanjo hiyo. Rais Uhuru Kenyatta mwenyewe ambaye ni mkatoliki amewakosoa wanaoipinga chanjo hiyo. "Tusisahau sayansi inasema nini kuhusu chanjo. Hata kama hatuwezi kuangamiza, angalau tunaweza kuipunguza kwa kuwalinda watoto na familia zetu," amesema. Wizara ya afya imeeleza kuwa dozi mbili za chanjo hiyo itatolewa katika kipindi cha miezi sita.

Ni mataifa gani yanayotoa chanjo dhidi ya HPV Afrika?

Mataifa kama Rwanda, Uganda, Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Ethiopia, Senegal, Malawi na sasa Kenya yameorodheshwa kwa mujibu wa shirika la afya duniani kuwa miongoni mwa mengine duniani yanayotoa chanjo hiyo ya HPV. Takwimu za Afrika na maeneo yanayopakana zinaeleza kuwa takriban watu 37,017 hufariki kila mwaka kutokana na saratani ya shingo ya kizazi katika eneo la Afrika mashariki pekee.

Rwanda imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuidhinisha chanjo ya HPV mnamo 2011 kwa mujibu wa WHO.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa UNICEF kufikiwa mwaka jana Desemba, Rwanda inawafikia zaidi ya 93% ya wasichana walio katika kidato cha sita na wa shule za msingi. Hatua hii imetajwa kutokana pakubwa na 'uwajibikaji wa serikali na mipango ya muda mrefu kusaidia kuimarisha afya na elimu ya wasichana na hatua ya kuwafikia kwa kushirikisha usajili wa shuleni na huduma ya afya.'

Serikali ya Tanzania pia imezindua kampeni ya chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi Aprili mwaka jana kama hatua ya kwanza ya kupambana na saratani Tanzania. Wakati huo mipango ililenga kuwachanja zaidi ya wasichana laki 6 walio na umri kati ya miaka 9 hadi 14 nchini.

"Saratani ya shingo ya kizazi ndio inayojitokeza zaidi Tanzania na ni chanzo cha vifo na magonjwa yanayohusiana na saratani miongoni mwa wanawake nchini."meneja wa mradi Daphrosa Lyimo aliiambia BBC wakati wa uzinduzi huo.

"Duniani, kuna zaidi ya wanawake 260,000 wanaofariki kwa sababu ya saratani hii, ambayo inazuilika na inatibiwa ikigunduliwa mapema." aliongezea Bwana Lyimo

Serikali imekuwa na matumaini kuwa kampeni hiyo itapunguza gharama za afya.Kumuuguza mgonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kunaweza kugharimu takriban dola za Marekani elfu 2 wakati 'dola 15 zitatumika kuwachanja wasichana' maafisa walisema.

Kukabiliana na dhana fiche kuhusu virusi vya HPV

Dhana: Unaweza kupata virusi vya HPV kwa njia ya kujamiiana pekee

Ukweli: HPV sana sana huenezwa kwa njia ya kujamiana lakini pia mtu anaweza kupata virusi hivyo kugusana kimwili hasa maeneo ya utupu na mtu aliye navyo.

Dhana: HPV ni inaashiria mtu ni mzinifu

Ukweli: 80% ya watu watapatikana na virusi vya HPV wakati mmoja katika maisha yao, ni rahisi kupata virusi hivyo na kuvisambaza kwa mto wa kwanza utakayefanya mapenzi nae.

Dhana: HPV inamaanisha niko na maradhi ya saratani

Ukweli: Kuna karibu aina 200 ya HPV. Karibu aina 40 ya virusi hivyo huathiri maeneo ya utupu, hii inamaananisha virusi hivyo vitaishi maeneo hayo ya mwili na baadhi ya virusi hivyo huenda vikasababisha magonjwa ya zinaa. Karibu aina 13 ya virusi hivyo huenda vikasababisa saratani ya shingo ya uzazi na aina nyingine ya saratani kama vile ya mdomo au koo lakini visa hivyo ni vichache.

Dhana: Utajua ikiwa una virusi vya HPV

Ukweli: HPV haina dalili zozote na wakati mwingine mfumo wa kinga ya mwili huweza kukabiliana na maambukizi. uchunguzi wa shingo ya uzazi unaweza kubaini seli zozote tumbo.

Saratani ya shingo ya uzazi ni nini?

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ambayo hutokea kwenye shingo ya kizazi cha mwanamke - ambayo ni kiingilio kutoka uke hadi katika mfuko wa uzazi. Ni moja kati ya zaidi ya aina 100 ya virusi vya human papilloma (HPV), ambavyo 13 vinasababisha saratani.

Pia aina fulani ya HPV vinaambukizwa kwa njia ya ngono.

Baadhi ya sababu za kupata ugonjwa huo ni kushiriki ngono ukiwa na umri mdogo, ukifanya ngono na washiriki wengi , kuvuta sigara na kuwa na virusi vya Ukimwi.

Dalili ni:

kupata hedhi kwa mzunguko usio wa kawaida au kutoka damu baada ya kujamiiana maumivu ya mgongo, mguu na fupanyonga uchovu, kupungua kwa uzito na kutokuwa na hamu ya kula maumivu kwenye uke au kutoa harufu mbaya kuvimba kwa mguu mmoja.

Uchunguzi wa virusi hivyo unastahili kufanyika ili kuvigundua mapema. Chanjo za HPV ni hatua nyingine ya kuziuzi. Matibabu kwa wagonjwa walio na virusi hivyo yanategemea na viwango vya virusi hivyo mwilini, hata hivyo yanaweza hitaji kutibiwa kwa njia ya upasuaji na kutoa sehemu au mfuko wa uzazi mzima au kutumia mionzi.

Chanzo: Shirika la Afya duniani