Raila Odinga amkejeli na kumfedhehesha Khalwale kwa tabia za kurusha mawe

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amemkejeli seneta wa zamani wa Kakamega Boni Khalwale baada ya picha zake kusambaa mtandaoni huku akiwa amejihami kwa mawe.

Khalwale ni miongoni mwa wanasiasa waliojipata taabani katika uchaguzi mdogo wa Kibra baada ya kushambuliwa na wahuni kwenye vurugu zilizoshuhudiwa.

Seneta huyo wa zamani ambaye alikuwa katika eneo hilo la Kibra ili 'kulinda' kura za mgombeaji wa Jubilee McDonald Mariga wakati alikabiliwa na wahuni hao katika uwanja wa DC.

Akiwashukuru wafuasi wake katika Kibra, Raila alimkejeli Khalwale huku akisema kwamba alikuwa mtaalamu wa mawe anayetafuta madini.

"Ametoka Ikolomani amekuja hapa Kibra kuwa geologist. Anachukua mawe hapa Kibra kutafuta gold,'' Raila alisema.

Kauli hiyo ya Raila kusema kwamba Khawale alikuwa mwanajiolojia ilichangamsha umati mkubwa uliokuwa umefurika uwanjani.

Naye gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alisema kwamba kile alichofanya Khalwale ni jambo la aibu kubwa kwa jamii ya Waluhya.

"Nimekuja kuomba msamaha kwa niaba ya watu wa kakamega kwa aibu mlizoonyeshwa hapa siku ya kupiga kura," alisema.

Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo alitoa wito kwa waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang'i kumkamata Khalwale kwa kushiriki katika vurugu hizo.

"Nilimwona Khalwale akibeba mawe na Matiang'i anafaa kuchukua hatua za kisheria bila kusita," Millie alisema.

Mbunge huyo wa Suba alimshtumu Khalwale kwa kueneza vurugu ulioshuhudiwa katika mchakato wa uchaguzi

"Ni yeye aliyeanzisha vurugu Kibra ilhali wakaazi walikuwa na amani siku hiyo,'' alisema.