Ruto amtaka DCI Kinoti kuharakisha upelelezi wa sakata ya jeshi    

RUTO ECHESA
RUTO ECHESA
Naibu rais William Ruto amemtaka DCI George Kinoti kuharakisha uchunguzi wa sakata ya silaha ya shilingi bilioni 39 inayodaiwa kumjumuisha aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa.

Kupitia msemaji wake David Mungonyi, Ruto alisema ofisi yake, Harambee Annex ilikuwa inashirikiana vyema na makachero.

“Mapema Ruto alikuwa amekejeli uchunguzi huo akisema kwamba unalenga kumchafulia jina na sasa ameamua kuunga Mkomo na kutaka ukamilike haraka iwekanavyo,” Mugonyi alisema.

Ruto alizungumza siku ambayo wakurugenzi wa kampuni moja ya Marekani walipelekwa katika jumba la Harambee Annex kuwatambua wafanyikazi wa Jumba hilo waliofanikisha mkutano wao na Echesa.

Wachunguzi kutoka idara ya DCI kitengo maalum cha uhalifu waliandamana na wakurugenzi wawili wa kampuni ya Eco Advanced Technologies hadi katika afisi ya naibu rais ambapo guaride ya kutambua wafanyikazi waliohusika ilifanywa.

Wakurugenzi wa kampuni yenye makao yake katika nchi za Marekani na Poland wamedai kulaghaiwa shilingi milioni 11.5 na Echesa, ili awasaidiye kupata zabuni ya shilingi bilioni 39.5 kutoka kwa idara ya jeshi.

Wachunguzi wanaamini kuwa Echesa alitumia hadhi ya afisi ya naibu rais kuwashawishi wawekezaji hao ili waamini uwezo wake kuwasaidia kupata zabuni hiyo. Hata hivyo, uhusiano wake na afisi ya naibu rais bado haujabainika.

Maafisa wa DCI walitumia muda mwingi jana, wakitathmini picha za CCTV na kuwahoji wafanyikazi na maafisa wa usalama katika afisi ya Ruto, ambayo sasa ni moja wapo wa maeneo ya uhalifu kuhusiana na zabuni gushi ya kijeshi.

Mkuu wa DCI George Kinoti alisema kwamba maafisa wake walikuwa bado wanakusanya ushahidi, huku aliyekuwa waziri Rashid Echesa na washukiwa wengine watatu wakishtakiwa kwa sakata ya zaidi ya shilingi bilioni 39, ambayo imeshtua wengi nchini.

Siku ya Jumatatu idara ya jeshi ilipinga kuhusika katika sakata hiyo. Pia inadaiwa kuwa Echesa alighushi saini ya waziri wa Ulinzi Monica Juma ili kudhihirishia wawakilishi wa kampuni ya Echo kwamba serikali ilikuwa imeidhinisha zabuni hiyo.

Wizara ya ulinzi ilisema kwamba maafisa wa uchunguzi na walalamishi walizuru makao makuu ya jeshi mjini Nairobi kumtambua afisa yeyote ambaye huenda walikutana naye.

"Wakati wa ziara hiyo, ilibainika kuwa walalamishi walikuwa hawajawahi kukutana na afisa yeyote wa jeshi aliye na mamlaka ya kuwakilisha wizara ya ulinzi,"Mkurugenzi wa mawasiliano wa KDF Bogita Ongeri alisema katika taarifa yake.

Aliongeza kwamba, "stakabadhi zote na malezo yaliowekwa kwa vyombo vya habari havikutoka kwa wizara ya ulinzi."

Siku ya Jumatatu Ruto alikanusha ripoti kuwa Echesa na walalamishi waliingia hadi eneo la kufanyia mikutano akisema kwamba hawakuruhusiwa kupita eneo la mapokezi katika afisi yake ya Harambee Annex.

Echesa na washukiwa wengine Daniel Otieno Omondi, Kennedy Oyoo Mboya na Clifford Okoth walifikishwa mahakamani siku ya Jumatatu na kukanusha mashtaka dhidi yao.

Kulingana na wachunguzi, watu watatu waliotambuliwa katika picha za CCTV wanafanya kazi katika afisi ya naibu rais iliyoko ghorofa ya pili huku mtu mwingine akiwa mwanasiasa mashuhuri.