Mwanamke asimulia kumuuza mwanawe kwa Ksh 20k ili kukata kiu yake ya uraibu wa pombe

“Mwanzoni alikuwa ananipa soda, kisha soda ikiwa imechanganywa na pombe kiasi na baadae akaanza kunipa pombe kavu. Hivyo ndivyo nilijikuta kwa uraibu wa pombe nikiwa na miaka 14,” Wanjiru alisimulia.

Muhtasari

• Wanjiru alisema kuwa mwanamke mmoja alimuunganisha na kakake ambaye alimtambulisha kwa vileo katika umri mdogo wa miaka 14.

Image: BBC

Mwanamke mmoja kutoka kaunti ya Murang’a amewashangaza wengi baada ya kutoa simulizi yake jinsi uraibu wa pombe ulimsukuma kuuza mwanawe kwa shilingi elfu 20 pekee ili kukidhi kiu yake ya pombe.

Katika simuliz yake kwa jarida la Nation, Wanjiru ambaye kwa sasa ni mwalimu wa ushauri nasaha katika kituo cha kurekebisha waraibu wa vileo huko Murang’a alieleza kwamba kabla ya kurekebika, alikuwa mraibu hatari wa vileo.

Katika simulizi yake, Wanjiru alisema alijikuta ameanza kutangamana na vikundi vya wanawake walevi baada ya kukosa nafasi ya kujiunga shule ya upili ya Alliance alikoitwa kutokana na ukosefu wa karo.

Wanjiru alisema kuwa mwanamke mmoja alimuunganisha na kakake ambaye alimtambulisha kwa vileo katika umri mdogo wa miaka 14.

“Mwanzoni alikuwa ananipa soda, kisha soda ikiwa imechanganywa na pombe kiasi na baadae akaanza kunipa pombe kavu. Hivyo ndivyo nilijikuta kwa uraibu wa pombe nikiwa na miaka 14,” Wanjiru alisimulia.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema kuwa huo ndio ulikuwa mwanzo wa safari yake ndefu na yenye changamoto nyingi, akifichua kwamba kwa wakati mmoja alijarbu kujikita katika biashara ya kujiuza kimwili na hata kujaribu kuiba katika maduka ya kuuza bidhaa.

“Siku moja nilishikwa nikiiba nikapigwa vibaya sana, baada ya hapo nilipelekwa seli na kushtakiwa kwa wizi. Kwa bahati nzuri, watu wa familia walinilipia dhamana na kunitoa jela. Pia niliiba kutoka kwa wanaume wengi, nilikuwa nawavizia wale wa mionekano ya kitajiri. Ningewatilia dawa kweney vinywaji vyao kabla ya kuwaibia. Nilitengeneza mamilioni ya pesa lakini pesa hizo hazikunisaidia hata kwa sababu ningeishia kuzitumia kwa kununua pombe na dawa za kulevya,” alinukuliwa na toleo hilo.

Kwa kuhofia kupelekwa jela tena, Wanjiru aliamua kurudi nyumbani kwao Kiharu kaunti ya Murang’a na huko, uraibu wake uliongezeka Zaidi kiasi kwamba alifikia hatua ya kumuuza mwanawe kwa elfu 20.

Hata hivyo, alipata kuona mwanga wa mabadiliko ya maisha yake 2015 wakati rais mstaafu Uhuru Kenyatta alitangaza msako dhidi ya vileo haramu ambapo gavana wa Murang’a kipindi hicho Mwangi wa Iria alianzisha kituo cha kurekebisha tabia za waraibu wa vileo.

Alijiunga katika kituo hicho na kurekebika kitabia na baadae kuwa mwalimu wa kuwasaidia wengine kurekebika dhidi ya vileo haramu.