Hata hivyo, shauku yake ilipanda zaidi wakati waliporejea bara, Eldoret na mume wake kuanza kufanya ziara za kushtukiza kurejea Pwani bila kueleza sababu za kuridhisha za ziara zake hizo . Mwanzoni alikuwa akisema kwamba alikuwa akienda kazi lakini Fidi alifahamu kwamba kazi yake ilikuwa ya afisa wa mifugo na alishangaa ilikuaje hadi akalazimika kwenda Malindi kila mara bila notisi .
Alipokuwa akienda Malindi, mume wake alikuwa akikatiza mawasiliano kabisa na ilikuwa vigumu kufahamu alikuwa eneo lipi hasa na alichokuwa akifanya. Siku moja Fidi alimuuliza kuhusu safari hizo na ndiposa ukweli ukadhihirika . Mume wake hakuwa na soni bali alimuambia kwamba alikuwa mpenzi wa jinsia moja a wakati akienda malindi , alikuwa akikutana na raia wa kigeni ambao pia walikuwa wapenzi wake. Fidi alivunjwa moyo kufahamu pale kwamba mume wake alikuwa kahaba wa kiume na kwanza kahaba wa jinsia moja .
Mume wake aliendelea kujitetea akisema kwamba alimuoa ili kuwafumba watu macho na kuepuka maswali ya jamaa na rafiki zake waliokuwa kila mara wanampa presha ya kupata mke . Mume wake alimuambia kwamba starehe zote walizokuwa wakizipata na yale maisha mazuri zilifadhiliwa na wazungu waliokuwa ‘wakifanya mapenzi’ naye na hivyo basi alikuwa na chaguo la kusalia katika ndoa yao au kuondoka na kukosa yote ‘mazuri’.
Fidi alichanganyikiwa asijiue kuomboleza hatua ya kufumbwa macho na mapenzi au ugunduzi kwamba aliolewa na mtu ambaye hakuwa na nia ya kumchukulia kama mke bali kama chombo cha kuficha alichokuwa akifanya. Hatimaye aliamua kujipa muda nje ya ndoa ili akitaraji kwamba mume wake angeweza kubadilika na kuachana na wapenzi wale wa kiume ili waanze upya maisha yao .